Wakati fulani Refa Mstaafu na maarufu Duniani, Pierluigi Collina aliulizwa kuhusu wakati wa kusisimua zaidi wa kazi yake uliowahi kutokea.
Collins alijibu kwa kusimulia kisa cha kusisimua akisema, “tulikuwa katika dakika mbili za mwisho, na niliwaona wachezaji wa Bayern wakiwa kwenye benchi tayari kusherehekea ubingwa wao. Mashabiki walikuwa wakikumbatiana kwenye viwanja wakisubiri filimbi yangu ya mwisho.”
Kisha ghafla, Manchester inafunga mabao mawili ndani ya dakika mbili na kurudisha nyuma matokeo. Sitasahau furaha ya wachezaji na benchi la Uingereza, ilionekana kama simba wakinguruma, mbele ya ukimya wa mashabiki wa Bayern.
Anasema wachezaji wa United walikuwa wakikimbia kama wendawazimu uwanjani, huku nikimwona mchezaji wa Bayern Samuel Kuffour amelala akilia bila tumaini na kukata tamaa.
“Nilimsogelea, lakini sikuweza kufikiria kitu kingine cha kumwambia zaidi ya “Amka upigane, bado una sekunde 20,” Collina alimpa matumaini Kuffour.
Anazidi kusimulia kwamba, “lakini wakati huo niliona sura halisi ya mpira wa miguu, ambapo wachezaji walijitolea maisha yao yote kwenye uwanja na watu wakipiga kelele kwa furaha na wengine wamejeruhiwa sana katika roho zao.”
Collina alikuwa akisimulia tukio la pambano la fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya mwaka 1999 kati ya Manchester United na Bayern Munich, mchezo uliofanyika katika jiji la Barcelona nchini Hispania.
Ipo hivi, kama ambavyo Manchester United hawakuona imeisha na kutokukata tamaa, basi ndivyo Collina aliona sekunde 20 zilitosha kubadilisha matokeo na akina Kuffour (Bayern) wangeweza kupata ushindi.
Hivyo, itumie vyema kila sekunde yako kwani inaweza kubadilisha matokeo ya jambo lolote katika mapambano yako ya kuyafikia mafanikio.