Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia ombi la wananchi wa Ngorongoro la kutumia haki hao ya Kikatiba ya kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa katika maeneo yao yaliyopo kwenye Tarafa ya Ngorongoro.
Lukuvi ametoa kauli hiyo Agosti 23, 2024 alipokuwa akizungumza na wananchi hao katika kijiji cha Kayapsi Kata ya Ngorongoro na Kijiji cha Irkepus kata ya Nainokanoka.
Amesema, uamuzi Mahakama wa kufuta Tamko ya Serikali la kufuta Kata, Vijiji na Vitongoji vilivyomo kwenye Tarafa ya Ngorongoro kushiriki kwenye uchaguzi huo limeongeze nguvu maelekezo ya Rais aliyokuwa ameyatoa kuwa wananchi waambiwe kuwa uchaguzi utafanyika wakiwa kwenye maeneo yao.
Aidha, Lukuvi amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro Murtallah Mboli kuendelea na maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwenye Vijiji 25 na Vitongoji 96 vya Tarafa hiyo.
“Mkurugenzi endelea na maandalizi yote muhimu ikiwa ni pamoja na kuhakiki maeneo ya mipaka, kuanisha maeneo ya kuandikishia wapiga kura pamoja na maeneo ya kupigia kura ili wananchi hawa waweze kushiriki kujiandikisha, kugombea nafasi za uongozi pamoja na kupiga kura ifikapo Novemba 27, 2024,” amesema.