Afarah Suleiman, Babati – Manyara.

Zaidi ya wapiga kura wapya milioni 5 laki 5 na 56 433 wanatarajiwa kujitokeza katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwenye zoezi la kujiandikisha katika uboreshwaji wa daftari la kudumu la mpiga kura na ambapo kwa mkoa wa Manyara watu laki 1 57 elfu 958 watajiandikisha katika daftari hilo.

Tume imeweka utaratibu kwa watu wenye ulemavu,wazee,wagonjwa, wajawazito na wakina mama wenye watoto wachanga watakaokwenda nao vituoni watapewa fursa ya kuhudumiwa bila kupanga foleni.

Akizungumza katika mkutano wa tume na wadau wa uchaguzi Mkoani Manyara Mjumbe wa Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Asina Omar amesema kwa yeyote mwenye sifa ya kujiandikisha katika daftari hilo anapaswa kujiandikisha mara Moja tu ili kuepuka uvunjwaji wa Sheria.

Amesema, “Mtu yeyote atakayeomba kuandikishwa zaidi ya mara moja atakuwa ametenda kosa la kisheria na akitiwa hatiani adhabu yake ni faini isiyopungua kiasi Cha shilingi laki moja na isiozidi Shilingi laki tatu au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili au vyote kwa pamoja.”

Aidha, Jaji Asina ameviomba vyama vya siasa pia kuwaamini mawakala wao ambao watakuepo vituoni kwaajili ya uboreshwaji wa daftari hilo ili kuepusha uvunjwaji wa Sheria huku akiwataka kuwahamasisha Wananchi kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Givness Aswile amesema viongozi wa dini mbalimbali wanawajibu pia kuwahamasisha waumini wao kujitokeza kwa wingi kwenye kujiandikisha katika daftari hilo kwakua ni haki ya Kila mtanzania mwenye sifa.

Nao baadhi ya washiriki wa mkutano huo akiwemo Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara Iddi Mkowa amesema vi vyema Kila chama kifuate utaratibu kwa mujibu wa Sheria na sio kuingilia majuku ya tume ya Uchaguzi huku Mwakilishi wa wanawake kwa Mkoa wa Manyara Veronica Peter ametoa hamasa wa jamii kushiriki kikamilifu katika uandikishwaji huo.

Zoezi la kujiandikisha uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura kwa mwaka 2024/2025 linabebwa na kauli mbiu isemayo, “KUJIANDIKISHA KUWA MPIGA KURA NI MSINGI WA UCHAGUZI BORA”.

Polisi: Kemeni ukatili, waleeni Watoto kimaadili
Picha: Matukio katika kilele cha Tamasha la Kizimkazi