Watu saba wanashikiliwa na Polisi, baada kupata miili mitatu nyumbani kwa Mganga wa kienyeji Namba Kasubi huko Mkoani Singida, huku miili miwili ikitambulika na mmoja bado haujatambulika.
Taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, Kamishna Msaidizi wa Polisi, DCP. David Misime aliyoitoa hii leo Agosti 26,2024 imeeleza kuwa Polisi walitoa taarifa ya matukio matatu ya Watu watatu kuripotiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha na baadaye kupatikana wakiwa wameuawa.
Matukio hayo yalikuwa ni ya Mikoa ya Singida, Dar es salaam na Tanga na baada ya kukamatwa Watuhumiwa Selemani Shabani Nyandalu maarufu kama Hango, Saidi Haji Msanghaa maarufu kama Mangu na Namba Kasubi ambaye ni Mganga wa kienyeji walionesha walikokuwa wamemfukia Samwaja Sifael Said baada ya kumuua, kukata sehemu zake za siri.
“Kwa msaada na ushirikiano mkubwa wa Wananchi, August 24,2024 mashimo mawili mengine yaliweza kubainika ambapo baada ya kufukuliwa ulipatikana mwili wa Gidion Samwel Mnyawi (53) Mkazi wa Makuro ambaye mara ya mwisho alionekana amepakizwa kwenye pikipiki na Watu wawili October 15,2023,” ilieleza taarifa hiyo.
“Mabaki ya mili ya Watu hao wawili yamebainika baada ya Wananchi na Askari kuoneshwa na Asha Bakari (51) Mkazi wa Migugu ambaye ni Mke wa Awadh Ramadhani maarufu Wawa (54 ) ambao ni Wakwe wa Nkamba Kasubi Mganga wa kienyeji ambao walikamatwa,”
“Chanzo cha Gidion kuuawa ni kutokana na kitendo chake cha kuuza shamba mara mbili, Hawa Mohamed Sumwa na Idd Hussein Idd walifikisha jambo hilo kwa Mganga huyo wa kienyeji naye akawaambia ili fedha zirudi inabidi Gidion Samwel atolewe kafara na ndipo mauaji hayo yakapangwa na kufanyika,” ilifafanua taarifa hiyo.