Mgonjwa wa 13 kupona ugonjwa wa sikoseli katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Jonester Peleka, mwenye umri wa 10, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa huduma ya matibabu.

Akiongea wakati wa dhifa ya kuruhusiwa BMH leo, Jonester, amesema anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kugharamia matibabu yake.

“Namshukuru pia Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali, Prof Makubi na timu yake yote kwa huduma hii. Nimehudumiwa vizuri toka nilipofika hapa,” amesema Jonester.

Kwa mujibu wa mama yake mzazi, Bahati Mbogo, alipokea taarifa kutoka kwa majirani zake kuwa Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Dodoma inatoa matibabu ya sikoseli.

“Majirani zangu waliona kwenye TV kuwa Hospitali ya Benjamin Mkapa wanatibu sikoseli ndiyo nikamleta mwanangu,” amesema Bi Bahati, ambaye ni mkazi wa Bigwa Kisiwani, Morogoro.

Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Damu BMH, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu, Stella Malangahe, amesema Jonester alipandikizwa uboho, ambayo ni matibabu ya sikoseli, tarehe 16 Julai, mwaka huu.

“Tumemruhusu mgonjwa wetu wa 13 kupona ugonjwa wa sikoseli siku ya leo. Tunawashukuru wazazi wake kwa kutuamini” amesema Daktari huyo Bingwa wa Magonjwa ya Damu, BMH.

Polisi watakiwa kuongeza udhibiti mabasi ya Wanafunzi
Serikali yapokea gawio la Bilioni 4.35 za TAZAMA