Serikali Nchini, imeiongezea bajeti Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) Wilaya ya Busega iliyopo mkoani Simiyu, kutoka shilingi milioni 500 hadi shilingi bilioni 2.4.

Hayo yameelezwa na Meneja wa TARURA Wilaya ya Busega, Mhandisi Mathias Mgolozi  mapema wiki hii aliyebainisha kuwa kutokana na nyongeza hiyo, TARURA  imekuwa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi nyingi, ambapo kwa mwaka 2023/24 wametengeneza kilomita 100 kati ya kilomita 511 walizonazo kwenye mtandao wa barabara wilayani humo.

Amesema, “miaka minne iliyopita wilaya ya Busega ilikuwa na bajeti ya shilingi milioni 500 kwa mwaka, baada ya kuingia madarakani Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan bajeti ya TARURA wilaya ya Busega imepanda kutoka milioni 500 hadi bilioni 2.4 kwa nyongeza ya tozo bilioni 1.2, mfuko wa jimbo milioni 500, na mfuko wa barabara milioni 748 na kufanya jumla ya bilioni 2.4.”

Ameitaja  miradi waliyotekeleza kuwa ni ujenzi wa daraja la Mwamanyili lenye upana  wa mita 20 kwa gharama ya shilingi milioni 121.6;   barabara ya Mwamigongwa kwenda Nyaluhande yenye urefu wa kilomita 6 pamoja na kufungua barabara mpya zenye urefu wa kilomita 4.8 kwa gharama ya shilingi milioni 237.

Miradi mingine iliyotekelezwa ni ujenzi wa madaraja matatu ya Mwamigongwa yenye upana wa mita 12, mita 8 na mita 6 kwa gharama ya shilingi milioni 477.

Naye, Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Nyaluhande, Robert Mabeyo amesema kwa mara ya kwanza ameona barabara zenye zaidi ya miaka 50 zikijengwa na TARURA kijijini hapo.

Wilaya ya Busega inaundwa na kata 15, TARURA wilaya ya Busega inahudumia barabara zenye urefu wa kilomita 511.10, na ina jumla ya barabara 136.

Ubadhirifu wa Miradi: Timu maalum kuwasili Kigoma
Uzinduzi Kampeni za Raila: Rais Samia awasili Kenya