Afarah Suleiman, Babati – Manyara.
Vijana wameaswa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika uboreshaji wa daftari la mpiga kura la Serikali za Mitaa kwa ajili kuchagua Viongozi wa Serikali za Mtaa utakaofanyika Novemba 27,2024.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga wakati akizungumzia na waandishi wa habari juu ya maandalizi ya Uchaguzi huo.
Amesema uandikishaji utaanza rasmi Septemba mosi mwaka huu ukiambatana na matembezi yatakayofanyika kwenye Wilaya zote Tano za Mkoa wa Manyara.
Amesema, Vijana wanapaswa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbli za uongozi pamoja na wanawake , kina mama wajitokeze kwa wingi kwakua watawakilisha sauti ya mama kuanzia ngazi ya chini.
Sendiga amesema, “wito wangu kwa Vijana nendeeni mkagombee,hesabu inaanza na Moja,kama unajiona wewe unasifa jitokeze,lakini sana wakina mama mkagombee,tunachangamoto sana kwenye Mkoa wetu katika lisha na ukatili,lakini tukiwa na kina mama wengi itanisaidia katika kupanga maendeleo.”
Aidha ameongeza kuwa ili kuhamasisha zoezi hilo la kujiandikisha Serikali ya Mkoa imeàmua kutumia michezo kwaajili ya kuunganisha Serikali na jamii ambapo Wananchi watakimbia au kutembea kilomita nane kwa mzunguko mzima pia itasaidia kuimarisha afya.
“Kwenye michezo tunauhakika tutakamata watu wa rika zote,maana michezo pia inahamasisha afya,michezo pia ni kiungo muhimu sana cha upashanaji habari kwaio ni muhimu sana,” alisema.
Amesema lila mtanzania anahaki ya kujiandikisha katika zoezi la uboreshaji wa daftari la mpiga kura la Serikali za Mitaa pamoja na kugombea kwenye nafasi za uongozi kuanzia Serikali za Mitaa hadi ngazi za juu.
Nao baadhi ya Vijana Mkoani Manyara akiwemo Lucas Alphonce amesema Vijana wanapaswa kuamka na kugombea katika nafasi mbalimbali ili kuleta hamasa ya maendeleo kwa Taifa huku Elisha Ako mazazi wa Hanang akiwashauri Vijana wenye vigezo vya kugombea katika nafasi mbalimbali wagombee kwa wingi.