Naibu Waziri, Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa -TAMISEMI, Zainab Katimba amesema Serikali inatambua umuhimu wa miundombinu ya Madaraja na inaendelea na urekebishaji wa madaraja yote ambayo yaliharibiwa na mvua zilizomalizika.
Katimba ameyasema hayo Bungeni Jijini Dodoma katika kipindi cha Maswali na Majibu wakati akijibu swali la mheshimiwa Anna Richard Lupembe mbunge wa jimbo la Nsimbo ambaye aliuliza Je, lini Serikali itajenga Daraja la Mafunsi Kata ya Itenka – Nsimbo.
Amesema kutokana na mvua za mwaka 2023/24 Wakala unapitia usanifu uliofanyika ili kujiridhisha kutokana na hali ya wingi wa maji uliobainika kwenye kipindi cha mvua za elinino. Kazi ya kupitia usanifu inaendelea kukamilishwa na inatarajia kukamilika mwezi wa Septemba, 2024 na mara itakapokamilka taratibu za ujenzi zitafuata.
Katimba ameongeza kuwa Serikali inafahamu umuhimu wa ujezi wa Daraja la Mafunsi Kata ya Itenka – Nsimbo, mwaka 2023/24 daraja hili lilifanyiwa usanifu ambapo gharama zinazohitajika zilikuwa Shilingi bilioni 2.3.