Polisi nchini Uganda, imesema mtu mmoja, Dhamulira Godfrey ambaye aliyekamatwa hivi karibuni akiwa na mafuvu 24 ya vichawa vya binadamu, huenda alikuwa anavitumia kwa utoaji kafara na endapo atakutwa na hatia atakabiliwa na kifungo cha maisha jela.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Uganda, Patrick Onyango amesema mtuhumiwa Dhamulira atashitakiwa chini ya sheria ya kuzuia na kudhibiti utoaji kafara za binadamu.
Amesema, baada ya kuchunguza makazi yake walipata mabaki ya Wanyama na ngozi, huku upekuzi ukiendelea kwani wanahisi huenda wakapata mabaki zaidi ya binadamu.
Hata hivyo, Godfrey ambaye alidai ni mganga wa jadi na tiba asilia, hajatambulika na Shirikisho la kitaifa la waganga wa jadi na tiba asilia la Uganda.
Hii si mara ya kwanza kwa tukio kama hilo, kwani ambapo mwezi Agosti walifanikiwa kupata mavufu 17 ya binadamu katika eneo la Mpigi, lililopo kilometa 41 kutokea jijini Kampala.