Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ametoa wito kwa Madaktari kuendelea kuwa na moyo wa huruma na upendo katika kuwahudumia wananchi kwa kuwa Mungu anawatumia wao katika kuponya magonjwa.

Ametoa rai hiyo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 87 wa mwaka wa Chama cha Madaktari Wakikristo Tanzania (Tanzania Christian Medical Association – TCMA) katika ukumbi wa mikutano wa St. Gaspar Dodoma.

 “Nimefurahi kusikia kwamba Chama chenu kinatimiza miaka 87 tangu kianzishwe kwake na kina jumla ya wananchama takribani 300 na hamjawahi kushindwa kukutana hata mara moja, huvyo mnapata fursa ya kujadili mambo muhimu kuhusu huduma za Afya na ustawi wa jamii yetu,” alisema Simbachawene.

Ameongeza kuwa, anafahamu katika msingi na Sera za Makanisa ya Kikiristo kuna utaratibu wa kuwasaidia wasiojiweza, hivyo ameomba taasisi hizo kuendelea na utaratibu huo, kwa kuwa Serikali iko pamoja nao wakati wote kwa manufaa ya umma.

Aidha, amezishauri taasisi hizo za kikiristo kutazama upya namna bora ya usimamizi Hospitali na vituo vyao vya afya kwa kuwa  sehemu nyingi kumekuwa na changamoto ya kushindwa kuviendesha vituo hivyo kutokana na watumishi wao kutoweka weledi katika kazi, kushindwa kwenda sambamba na mahitaji ya wateja na ukuaji wa sayansi na teknolojia.

Awali,  Rais wa Chama cha Madaktari Wakikristo Tanzania (TCMA), Gresmus Ssebuyoya amesema wanachama hao hukutana kila mwaka kwa lengo la kubadilisha uzoefu, kujifunza na kuainisha changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa shughuli, kuziweka pamoja na kuziwasilisha kwa Maaskofu kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi.

“Chama kiko tayari na kitaendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa huduma za afya kwa wananchi na kuboresha huduma za afya kwa watu wenye uwezo mdogo wa kumudu gharama za afya” Amesema Ssebuyoya.

Kaulimbiu ya mkutano wa 87 wa chama hicho kwa mwaka 2024 ni “The future of healthcare: Innovation and solution for future”  ikilenga kuwasaidia madaktari katika kujiiandaa na kutekeleza wa mkakati wa utoaji wa huduma ya afya kwa wote na kukabiliana na mazingira ya utoaji wa huduma za Afya ambayo yanabadilika haraka na kuongezeka kwa malalamiko ya kukosekana kwa maadili kwa watumishi wa afya nchini.

EWURA yatangaza bei kikomo za Mafuta
Dkt. Mfaume ataka uwajibikaji sekta ya Afya