Waziri, Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Uchukuzi iendelee kulisimamia kwa karibu Shirika la Reli Tanzania (TRC) na kuhakikisha huduma za treni ya SGR zinaboreshwa na miundombinu inaimarishwa ili mradi huo uweze kudumu kwa muda mrefu.

Majaliwa ameyasema hayo hii leo Septemba 6, 2024 wakati wa kuahirisha Mkutano wa 16 wa Bunge, jijini Dodoma na kudai kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali itaendeleza sekta ya uchukuzi ambapo pamoja na mambo mengine itasimamia sekta ya reli ikiwemo ujenzi wa SGR na uendeshaji wa treni ya kisasa ya abiria kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.

 

Amesema, Desemba 31, 2023 Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alielekeza kuanza uendeshaji wa reli ya SGR kwa kipande cha Dar es Salaam – Dodoma ifikapo mwezi Julai, 2024.

 “Naomba kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa, safari za treni ya mwendokasi kutoka Dar es Salaam – Morogoro zilianza tarehe 14 Juni 2024 na tarehe 25 Julai 2024 uendeshaji wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ulianza,” alifafanua Waziri Mkuu.

Aidha Majaliwa ameongeza kuwa, Agosti 1, 2024 Dkt. Samia Suluhu Hassan pia alizindua utoaji wa huduma za reli ya kisasa ya SGR kutoka jiji la Dar es salaam kupitia Mkoa wa Morogoro hadi Jiji la Dodoma.

Amesema, treni hiyo inaendelea kutoa huduma kwa wananchi na imechangia kuimarisha sekta ya usafirishaji. “Kipekee ninaomba kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia maono yake na kwa kweli anaahidi, anatekeleza, Kazi Iendelee”.

Wizara yatakiwa kisimamia upatikanaji pembejeo za kilimo
Tanzania yatoa somo uzalishaji, matumizi ya Nishati