Ancelotti ni mmoja wa makocha waliopambwa zaidi katika historia ya soka barani Ulaya, mataji yake matano ya UEFA Champions League yanamfanya kocha huyo kuwa na rekodi ya kipekee kwenye mashindano hayo.Ancelloti alitwaa taji la tano akiwa kocha Real Madrid mwezi Juni walipoichapa Borussia Dortmund katika fainali iliyofanyika Uwanja wa Wembley,
Ancelotti mara nyingi anaonekana kuwa kisiwa cha utulivu huku kukiwa na machafuko, lakini Muitaliano huyo anasisitiza kuwa bado ana wasiwasi kabla ya mechi kubwa na atafanya hivyo hadi siku atakapostaafu. Kocha huyo amenukuliwa akisema
“Maisha bila presha au stress kidogo hayapo, stress nyingi.Kabla ya mechi kuna wasiwasi, kuna hisia hasi ukifikiri kwamba haitaenda vizuri, kwamba watafunga bao … Wakati mechi inaanza, kila kitu kinasimama.Kwa hiyo, mnatakiwa kutafuta utulivu ili kushughulikia hali ya mchezo, nitaendelea kufundisha hadi moto nilionao wa soka utakapozimika.
“Kuna mambo makubwa yametokea katika maisha yangu, nyakati ngumu, maisha yangu yamekuwa ya kawaida, nimepata bahati ya kupata kazi ambayo ni mapenzi yangu, nashukuru soka kwa kunipa nafasi hiyo.
“Bado napata woga kabla ya mechi, ninahisi shinikizo, na mradi tu hilo halibadiliki nitaendelea kuwa hapa. Ninajiona ninafundisha kwa muda mrefu.”
Ancelotti anajulikana kwa kuwashirikisha wachezaji wake wenye majina makubwa katika kufanya maamuzi yake, na anasema kuwa mbinu ya ushirikiano imekuwa ufunguo wa mafanikio yake.
“Ni vigumu sana kueleza jinsi kiongozi anapaswa kuwa. Ni muhimu zaidi kuwashawishi kuliko kulazimisha maoni yako kwao,” aliongeza.
“Kiongozi lazima awe na uwezo wa kuwasikiliza wanaofanya kazi na wewe, wanaweza kukupa mawazo ambayo yanaweza kukusaidia.
“Ni muhimu kusikiliza na sio kufikiria kuwa unajua kila kitu kwa sababu wewe ndiye bosi. Unaweza kujifunza kila wakati.”