Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imetupilia mbali rufaa ya Juma Ally Magoma na mwenzake Geofrey Mwaipopo waliyokuwa wameikata dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Klabu ya Yanga.Uamuzi huo ulitolewa Jumatatu, Septemba 9, 2024 na Naibu wa Mahakama hiyo, Livini Lyakinana kwa niaba ya Jaji Mfawidhi, Salma Maghimbi aliyeisikiliza rufaa hiyo.
Magoma na Mwaipopo walikata rufaa hiyo mahakamani hapo wakipinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu kuiongezea Bodi ya Wadhamini ya Klabu ya Yanga na wenzake muda wa kufungua shauri la maombi ya marejeo.
Yanga iliomba kuongezewa muda huo ili kufungua shauri hilo la marejeo ya hukumu ya mahakama hiyo iliyobatilisha Katiba yake ya sasa kufuatia kesi ya msingi iliyofunguliwa na Magoma na mwenzake, wakihoji uhalali wa katiba hiyo.
Wajibu rufaa katika rufaa hiyo walikuwa ni Bodi ya Wadhamini ya Klabu ya Yanga (mjibu rufaa wa kwanza), Fatma Abeid Karume (mjumbe wa bodi hiyo mpaka sasa), Abeid Abeid na Jabiri Katundu, ambao pia waliwahi kuwa wajumbe wa bodi ya klabu hiyo.
Bodi ya wadhamini wa Yanga imewawekea pingamizi la hoja za kisheria kina Magoma dhidi ya rufaa hiyo, ikibainisha hoja mbili. Kwanza inadai kuwa uamuzi ambao kina Magoma wameukatia rufaa na ya pili wanadai kuwa rufaa hiyo imeshapitwa na tukio.
Pingamizi hilo lilisikilizwa Agosti 30 mwaka huu, ambapo mawakili pande zote Kalaghe Rashid wa Yanga na Jacob Mashenene wa kina Magoma walichuana kwa hoja za kisheria kila mmoja akijitahidi kuishaiwishi mahakama ikubaliane nao na kurejea kesi mbalimbali kusisitiza hoja zao.
Hata hivyo Mahakama katika uamuzi wake imetupilia mbali rufaa hiyo baada ya kukubaliana na pingamizi la Yanga kuwa uamuzi waliokuwa wanaukatia rufaa haukuapaswa kukatiwa rufaa kwa mujibu wa Sheria.
Jaji Maghimbi amefikia hitimisho hilo baada ya kuzingatia hoja hiyo moja tu ya pingamizi Yanga, kuwa uamuzi huo haukatiwi rufaa ambayo imetosha kumaliza shauri hilo.
“Rufaa hii inakiuka Amri ya 74 (2) ya Sheria ya Mwenendo wa Madai. Kwa hiyo Mahakama haiwezi kusikiliza rufaa inayotokana na uamuzi usiokatiwa rufaa. Hivyo inaifuta rufaa hii,” amesema Naibu Msajili Lyakinana akimnukuu Jaji Maghimbi.
Akisoma uamuzi huo, Naibu Msajili Lyakinana amesema kwa kuwa sababu hiyo imetosha kumaliza shauri hilo hana sababu ya kuendelea na uamuzi wa sababu nyingine ya pingamizi.
Kuhusu gharama za uendeshaji wa shauri hilo, mahakama hiyo imesema kutokana na mahusiano ya wadaawa inaamuru kila upande ubebe gharama zake.
Akizungumzia uamuzi huo, Wakili wa Yanga, Kalaghe Rashid amesema wanaamini mahakama imetenda haki kwa kuwa imesema wazi kisheria uamuzi kama huo ambao haiamui haki za msingi za wadaawa kama huo waliokuwa wakiukatia rufaa kina Magoma haupaswi kukatiwa rufaa.
Hata hivyo kwa upande wake Wakili wa kina Magoma, Jacob Mashenene amesema kuwa wanasubiri kupata nakala ya uamuzi huo ili waipitie kuona kama wanaweza kuchukua hatua zaidi au la, akisema kuwa mahakama hiyo si ya uamuzi wa mwisho.
Chimbuko la rufaa hiyo ni kesi iliyofunguliwa na Magoma na Mwaipopo Agosti 4, 2022, wakipinga Katiba hiyo ya mwaka 2011 kuwa si halali kisheria na kwamba Katiba halali inayotambulika ni ile ya mwaka 1968.
Hivyo waliiomba mahakama hiyo itamke kuwa Katiba ya mwaka 2011 ni batili na wajumbe wa bodi waliopo kwa Katiba ya sasa hawana uhalali na miamala yote ya kifedha waliyoifanya ni batili.
Kesi hiyo ilisikilizwa na Hakimu Pamela Mazengo, upande mmoja bila wadaiwa wengine kuwepo isipokuwa Abeid pekee, kwa madai kuwa walipelekewa wito wa Mahakama lakini hawakuitikia.
Mahakama hiyo katika uamuzi wake Agosti 2, 2023, ilikubaliana na hoja za kina Magoma, ikabatilisha Katiba ya sasa ya Yanga ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2011, kuwa haitambuliki kisheria na kwamba Katiba halali ya klabu hiyo ni ya mwaka 1968.
Pia ilisema kuwa hivyo Bodi ya Wadhamini wa klabu hiyo iliyoingia madarakani kwa Katiba ya mwaka 2011 si halali na chochote kilichofanywa na bodi hiyo ni batili na ikaamuru Bodi ya Wadhamini ya mwaka 1968 ndio irejeshwe katika uongozi kuendesha klabu hiyo.
Pia mahakama hiyo iliamuru kuwa miamala yote ya kifedha iliyofanywa na Bodi ya Wadhamini wa Klabu hiyo iliyoingia madarakani kwa Katiba ya sasa ni batili.
Wajumbe wa Bodi ya wadhamini wa Yanga kwa sasa ni George Mkuchika (mwenyekiti), Fatma Abeid Aman Karume, Dk Mwigulu Lameck Nchemba, Tarimba Abbas na Anthony Mavunde.
Hukumu hiyo iliibuka Julai 16, 2024, mwaka mmoja baadaye kupitia vyombo vya habari likiwemo Mwananchi, baada ya walalamikaji hao kurudi mahakamani kuomba utekelezaji wa hukumu hiyo.
Uongozi wa klabu hiyo, kupitia Mkurugenzi wake wa Sheria, Wakili Simon Patrick ulieleza kuwa hakuwa unafahamu kuwepo kwa kesi na hukumu hiyo. Mpaka wakati huo ilipoupata uamuzi huo ilikuwa imeshachelewa kuchukua hatua zozote za kuupinga.
Hivyo ililazimika kuomba kuruhusiwa kufungua shauri la maombi ya marejeo kupinga hukumu hiyo nje ya muda, ikakubaliwa ndipo wakafungua maombi haya ya marejeo.
Kufuatia uamuzi huo ndipo kina Magoma wakakata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo.
Hata hivyo Agosti 5, 2024, Mahakama ya Kisutu ilisikiliza shauri la maombi ya marejeo la Wadhamini wa Yanga na katika uamuzi wake ilioutoa Agosti 9, 2024, Mahakama hiyo ilikubaliaa na hoja za Yanga ikatengua hukumu yaka ya awali iliyokuwa imebatilisha Katiba ya Yanga ya sasa.