Heldina Mwingira – Dar24 Media.
Kuna njia nyingi za utafutaji katika maisha, ambazo zote hulenga nia moja ya kufanikisha upataji wa mkate wa kila siku na kumudu maisha.
Binadamu hutafuta kazi na sote tunatambua kwamba njia hiyo ndiyo pekee ya kujipatia ujira tena bila kuchagua, ili mradi mkono uende kinywani.
Kuna hii ya urembo wa kucha ambayo nayo inatamba sana ikionekana ni fursa katika maisha ya vijana wengi, hasa wa miji mikubwa kama Dar es Salaam nk.
Biashara hii ni mahsusi kwa ajili ya kuwahudumia Wanawake kwa kupakwa rangi, kusafishwa kucha, kuoshwa miguu ingawa wapo pia wanaume ambao nao hupendelea kusafisha kucha na miguu.
Hata hivyo, inaarifiwa kuwa njia hii ya kuwahudumia Wanawake kwa urembo na usafi wa kucha imekuwa ikivuka mipaka ikidaiwa kuvunja maadili ya Kitanzania, yaani kupitia biashara hiyo mfanyabiashara (mpaka rangi) na mteja (mpakwa rangi) huingia katika mahusiano.
Kutokana na sintofahamu ya suala hilo, Dar24 Media ililazimika kufanya mahojiano na baadhi ya watu katika jamii, ili kupata ukweli wa suala hilo, ambapo Joseph Innocent (mfanyabishara jirani na mpaka rangi) alisimulia jambo.
Anasema, “naonaga wadada na Wanawake tofauti tofauti wanakuja kila siku hapa kupakwa rangi, na katika harakati za kupata huduma ndipo wanapotongozana na kupatiana namba kwa ajili ya makutano ya baadae, kwa upande wangu naona mara nyingi Wanawake hupenda kubandika hizo kucha wakiwa wamevaa sketi fupi na husafishwa mpaka maeneo ya mapajani na hivyo hupelekea mtengeneza kucha na wao wote kupata tamaa.”
“Hivi viumbe vya kike ni rahisi kupata ushawishi hivyo anaweza ukawa hajafikiria kufanya mapenzi lakini katika hali ya kushikwashikwa miguu anajikuta akimvumtia hisia mtu anayemshika na pengine haridhishwi au hapati huduma mara kwa mara kutoka kwa mpenzi wake,” alifafanua Joseph.
Omari Juma, yeye ni mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam yeye alisema, “Siwezi mruhusu mke wangu abadani, kwa upande wangu huwa najiuliza, mwanaume unamruhusu vipi mkeo au mtu unayempenda kwenda kupata huduma hii? Kwani hawezi kujisafisha mwenyewe akiwa nyumbani?.”
“Siwezi mruhusu Mwanaume mwingine amshike na kumpapasa mke wangu kiungo chochote, kwa hiyo hata kupaka kucha rangi, huwa namuambia jipake mwenyewe au aachane nazo sio lazima ninayoyaona mimi na kuyasikia, ni kwamba Wanawake hujipanga mstari, kupakwa rangi kucha na kuoshwa miguu huwa najiuliza ni urembo tu au kuna kitu kingine cha ziada?,” alihoji Omari.
Hata hivyo, wapo Wanaume wanaowaruhusu wake au wapenzi wao kupata huduma hiyo mmoja wao akiwa ni Said Juma, yeye anasema huwa anamruhusu akiamini ni njia mojawapo ya urembo na kuhusu kuanzisha mahusiano, hiyo ni tabia binafsi ya mtu.
Dar24 Media pia ilitaka kujua Wanawake wanasemaje kuhusiana na suala hili, ndipo ilimpata Irene John akisema, “jamani kupakwa rangi na kusuguliwa miguu ni usmart na urembo tu kwa mwanamke na sio vinginevyo kama jamii inavyofikiria.”
Hata hivyo, anakiri kwamba baadhi ya vijana huwa wanatumia nafasi hiyo ya kuwasafisha, kwa kuwatekenya na kuwapapasa Wanawake sehemu za miguu na mapajani, ili iwe rahisi kuwarubuni kihisia.
Hapa mpaka rangi ilibidi ahusishwe kudadavua undani wa madai haya, ndipo akapatikana John Raphael ambaye alijiweka kiofisi zaidi.
Anasema, “sisi ofisi yetu tunamtafsiri mwanamke yeyote anayekuja kupaka rangi ni mteja sio vnginevyo kwa sababu tukianza kuhusisha mahusiano tutakosa hela, hii ni kazi kama kazi nyingine ukiheshimu nayo itakuheshimu itakuongezea kipato.”
John anasema wakati mwingine wao hupata wateja Wanawake wenye heshima na vyeo vyao, hivyo hawawezi kujiharibia na kukimbiwa na wateja kwa sababu ya tamaa za dakika chache.
Kuhusu changamoto zinazowakabili kutokana na mtazamo wa kijamii wa biashara John anabainisha kuwa mtazamo wa jamii hupelekea wao kupata changamoto kama vile kupungua kwa wateja kwani Wanawake huogopa kwenda kupata huduma, kwasababu wamesikia habari mbaya za ujumla na wanaume hukataza Wanawake zao kwa kuogopa kusalitiwa.”
“Ila Siku hizi na watu kidogo wameanza kuelewa na wengine wakiona vipi Wanaume wanawasindikiza wake au wapenzi wao na wanasubiri palepale mpaka tunamalizia kuwapaka rangi,” anafafanua John.
Kutokana na mitazamo ya kijamii, hupelekea kazi hii kuonekana yenye ukosefu wa maadili ndani yake, lakini ni muhimu ieleweke kuwa hiyo halali ya kujipatia ujira na si wote wenye tabia kama hizo.
Tuzidi kuunga mkono juhudi za Vijana pale inapotokea wanajiajiri wenyewe kwa kazi halali na kujipatia kipato na pale inaotokea kuna jambo linaonekana walakini tusisite kuwashauri ili waweze kuboresha kazi zao na wakaziheshimu pia.