Mkazi wa Lindi, Karume Karume (41) aliyesumbuliwa na uvimbe sehemu mbalimbali za mwili wake kwa zaidi ya miaka 25, leo ameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kufanikiwa kufanyiwa upasuaji rekebishi na watalaam wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuondolewa uvimbe wenye uzito wa kilo tano.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Bingwa Mbobezi wa Upasuaji Rekebishi na Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji Rekebishi, Dkt. Laurean Rwanyuma aliyeongoza jopo la watalaam wenzake kumfanyia upasuaji uliodumu kwa saa nne, amesema baada ya uchunguzi wa kina kukamilika, iligundulika kuwa Karume ana uvimbe.

Uvimbe huo ulikuwa sehemu mbalimbali za mwili wake hasa shingoni, begani na kifuani na kwamba ugonjwa huo unaitwa Plexiform Neurofibromatosis ambao matibabu yake ni kuondolewa kwa njia ya upasuaji ambapo Agosti 30, 2024 alifanyiwa upasuaji.

Amesema, ugonjwa aliopata Karume siyo wa kuambukiza bali ni ugonjwa wa kuzaliwa nao ambao ameurithi kutoka kwa ama mmoja wa wazazi wake au wazazi wake wawili wenye ugonjwa huo ambao hushambulia mishipa ya fahamu na kujitokeza kwa njia mbalimbali.

Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dkt. Rachel Mhaville akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, amesema mara baada ya kumpokea Karume Agosti 2024, Hospitali ilifanya jitihada za dhati kuhakikisha anaonwa na madaktari bingwa na kumfanyia vipimo mbalimbali.

 

Walifanya hivyo, ili kubaini mwenendo wa matibabu yake na kuwapongeza waandishi wa habari kumuibua mgonjwa huyo na kumleta hospitalini hapo kwani ndipo penye madaktari bingwa bobezi wa upasuaji rekebishi walioweza kumpa huduma stahiki na kumrejeshea mwonekano unaompa faraja na tabasamu.

Dkt. Mhaville amewaomba wasamaria wema kuendelea kujitokeza kuchangia huduma kwa watu wasiokuwa na uwezo akiwemo Bw. Karume ili kukamilisha malipo ya huduma alizopata kupitia namba ya malipo 994501766575 yenye jina Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Kwa upande wake, mjomba wa Karume, Salum Ahamad Idobelele amesema alianza kuangaika na Karume akiwa na miaka 16 baada ya kupata uvimbe huo na baadae kubahatika kukutana na Waandishi kupitia Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam ambao walibeba jukumu la kumtafutia msaada wa matibabu kwa kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke na kisha kupewa rufaa ya kwendavHospitali ya Taifa Muhimbili.

SMZ kutekeleza mkakati uwezeshaji Wananchi kiuchumi