Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ametoa rai kwa vijana nchini kuwa na mshikamano na kudumisha amani iliyopo nchini kwani tunu hiyo kwa Tanzania na Dunia kiujumla ipo mikononi mwa Vijana.

Dkt. Biteko rai hiyo jijini Dar es salaam wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa la Ajenda ya Amani na Usalama kwa Vijana.

“Wito wangu kwenu shikamaneni shikamaneni shikamaneni! kwa ajili ya kulinda amani ya nchi yetu ili tuwe na Taifa la utulivu na tufurahie maisha yetu, ni vizuri mkakumbuka kuwa hiki ni kipindi cha kujiandaa kuwa baba bora au mke mwema ili baadae kuwa na Taifa bora,’’ amesisitiza Dkt. Biteko.

Akizungumzia maendeleo ya utandawazi na mapinduzi makubwa ya kidijitali ambayo yamekuwa yakitoa fursa lukuki kwa Vijana, Dkt. Biteko amesema, ‘’Napenda kuwaasa kwamba matumizi ya teknolojia yakawe na malengo ya kuzalisha na kujitengenezea kipato endelevu, kwa kufanya hivyo kutakuza uchumi na kuonyesha tija ya nguvu kazi yetu katika Taifa letu. Aidha, siyo teknolojia hii inavyotumika sasa kama majukwaa ya uhalifu, uchochezi, udhalilishaji wa kijinsia na uvunjaji wa amani iliyojengwa na vizazi vya Watanzania wengi. Natamani Baada ya Kongamano hili nyie wote mlioudhuria hapa mkawe chachu kwa vijana wenzenu mtakao kutana nao, mkawe dira na walimu bora wa amani,’’ amesema.

Aidha, Dkt. Biteko ameongeza kuwa katika kuhakikisha kunakuwepo na mazingira mazuri ya ushiriki na ushikikishwaji wa vijana katika masuala mbalimbali ya maendeleo Serikali imefanyia maboresho Sera ya zamani Maendeleo ya Vijana na tarehe 12 Agosti 2014 Sera Mpya ya Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007, tolea la mwaka 2024 ilizinduliwa.

‘’Sera hii imeeleza nia ya dhati ya Serikali kuhakikisha vijana wanaandaliwa kuwa wazalendo, waadilifu na wanaoshiriki kudumisha amani na usalama wa nchi yetu. Hii yote ni kutambua umuhimu na nguvu waliyonayo vijana na umuhimu wa ushirikishwaji wao katika katika kujenga nchi yetu. Katika kipindi hiki ambacho nchi yetu ipo katika mchakato wa kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ninawasihi kuwa tumieni fursa hii kuhakikisha mnatoa maoni yenu ambayo pamoja na mambo mengine yatawezesha ushirikishwaji wa vijana kwenye kwenye maendeleo, lakini hasa katika misingi ya amani na usalama na mtumie ubunifu wenu kupendekeza mikakati rafiki kwa vijana itakayowawezesha kushiriki kujenga aina ya Tanzania tuitakayo miaka 25 ijayo,’’ amesisitiza Dkt. Biteko.

‘’Wote mtakuwa mashahidi kinachoendelea duniani kote, amani imepungua, vifo vimeongezeka, matukio ya uovu yamekithiri na baadhi ya mataifa hayana amani kwa sababu yana migogoro na mivutano ya kisiasa. Ni vyema mkatambua kwamba ninyi vijana wa Tanzania pamoja na wenzenu duniani kote mna jukumu kubwa la kutoa hamasa ya kushiriki katika kujenga na kuilinda amani, na msimruhusu mtu yoyote kuichezea tunu hiyo muhimu kwenye mustakabali wa Taifa lolote Duniani,’’ alisema Dkt. Biteko.

Kwa upande wake, Msimamizi Mkuu wa Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Tanzania, Shabnam Malick amesema kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kufadhili programu mbalimbali kuhusu vijana kwa kuwa vijana wana mchango mkubwa katika kuleta maendeleo nchini.

‘’Tunaamini kuwa amani ni nguzo muhimu ya maendeleo na msingi wa maendeleo endelevu ni lazima tushirikishe vijana katika kufanya maamuzi,’’ amesema Malick.

Naye, Mkurugenzi wa Shirika la A.L.I.I na Mratibu wa Kongamano hilo la Vijana, Joseph Malekelea amesema kuwa Kongamano hilo limefanyika kuendana na maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani linalofanyika Septemba 21 kila mwaka lilianzishwa mwaka 1981 kwa lengo la kukumbusha watu, mataifa na wadau mbalimbali umuhimu wa kudumisha maadili ya amani na usalama.

‘’Tanzania tumekuwa tukiadhimisha siku hiyo na kwa ubunifu wetu tukamua kuandaa Kongamano hili ili tuweze kuona kwa kina je vijana wetu wanaelewa kuhusiana na amani, je wanashiriki katika kudumisha amani katika nchi yetu, je vijana wetu wanashirikishwa katika suala zima la amani, kipi kifanyike kuhakikisha vijana wanakuwa mstari wa mbele katika kudumisha amani,’’ amesema Malekela.

Kongamano hilo lenye kaulimbiu “KIJANA CHUKUA HATUA KUDUMISHA UTAMADUNI WA AMANI TANZANIA.” Limefanyika sambamba na utoaji wa elimu katika shule mbalimbali kuhusu kudumisha utamaduni wa amani kupitia midahalo ya vijana na mbio za amani katika mikoa ya Tanga, Mjini Magaribi – Zanzibar, Pwani, Lindi na Mtwara na kuwafikia zaidi ya vijana 10,000.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Septemba 23, 2024
Zoezi ubainishaji Watoto wenye mahitaji maalum kuendelezwa