Kocha Miguel Gamondi amepiga mkwara mpya akisema kwa sasa wao ni mwendo mdundo tu hadi kieleweke.Mkwara huo mpya wa Gamondi ameupiga wakati akijiandaa sasa kurudisha shoo katika Ligi Kuu Bara ili kuanza kutetea taji inalolishikilia kwa msimu wa tatu mfululizo na la 30 tangu ligi ilipoanza mwaka 1965.
Kocha huyo aliyetwaa taji hilo katika msimu wa kwanza tangu ajiunge na Yanga, huku akiiwezesha pia timu hiyo kutetea ubingwa wa Kombe la Shirikisho kwa msimu wa tatu mfululizo na msimu huu tayari ameshatia kibindoni Ngao ya Jamii akiifanyizia Azam FC katika fainali kwa kuilaza 4-1.
Gamondi ambaye msimu uliopita katika ligi hiyo alitembeza vichapo vya maana kwa ushindi wa mabao matano kwenye mechi nne tofauti ikiwemo dhidi ya Simba waliyoifumua mabao 5-1, aliliambia Mwanaspoti anataka kuona kila nafasi wanayoipata inageuzwa kuwa bao kwani tayari amewapa mbinu bora wachezaji.
Raia huyo wa Argentina, baada ya kukamilisha hilo huku akibainisha mchezo wa jana dhidi ya CBE aliingia kama sehemu ya kuangalia kile alichofundisha kama kimeanza kufanya kazi, amepanga kuendeleza balaa hilo katika ligi.
Ikumbukwe katika raundi tano za ligi hadi sasa, Yanga ndiyo timu pekee iliyocheza mechi moja tu na ilianza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar na baada ya kumalizana na Wahabeshi, itasafiri hadi Mbeya katikati ya wiki kuvaana na KenGold iliyopanda daraja msimu huu.
Kucheza mechi moja tu kwa Yanga kulitokana na majukumu ya michuano ya kimataifa kwani ilianza raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiifumua Vital’O ya Burundi jumla ya mabao 10-0 katika michezo miwili kabla ya kushinda 1-0 ugenini dhidi ya CBE iliyokuwa ikimalizana nao jana usiku mjini Unguja.
Baada ya kumaliza mechi hiyo ya jana ambayo Yanga ilikuwa ikihitaji sare yoyote kuandika rekodi mpya ya kutinga hatua ya makundi misimu miwili mfululizo baada ya msimu uliopita kufanya hivyo ikiwa imepita miaka 25 tangu ilipocheza hatua kama hiyo mwaka 1998, Jumatano itaifuata KenGold jijini Mbeya.
“Naamini kwa sasa kiwango chetu cha kufunga mabao kinaendelea kuimarika, imani yangu ni tutazidi kuwa bora katika mechi zilizo mbele yetu. Malengo ni kutaka kuona kila nafasi tunaigeuza kuwa bao kwani hakuna timu inayopata ushindi bila ya kufunga mabao, wachezaji wangu wanalielewa hilo,” alisema Gamondi ambaye msimu uliopita aliifikisha Yanga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kauli hiyo ya Gamondi ni wazi anataka salamu ziwafikie KenGold iliyopoteza mechi zote nne za Ligi Kuu Bara inayoicheza kwa mara ya kwanza msimu huu, huku ikifunga mabao mawili na kufungwa manane, kitu kinacholifanya benchi la ufundi la timu hiyo ya Mbeya kuanza kukuna vichwa mapema kabla ya kuvaana.
Katika mechi ya kwanza dhidi ya Singida BS, timu hiyo ilichapwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Sokoine, kisha kwenda kulala 2-1 ugenini dhidi ya Fountain Gate kabla ya kulazwa1-0 na KMC na juzi usiku ikacharazwa tena 2-0 na Kagera Sugar ikiwa pia ugenini.