Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamisha Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Muliro Jumanne amewataka Wananchi kutokuwa na hofu na badala yake waendelee na shughuli zao mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwani ulinzi umeendelea kuimarishwa ili mali zao kuwa salama.
Muliro ameyasema hayo hii leo Septemba 23, 2024 wakati akizungumza na Vyombo vya Habari na kuongeza kuwa wito huo unatokana na uwepo wa jaribio la maandamano yaliyokuwa yakiratibiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA ambayo yalipigwa marufuku akidai yasingekuwa ya amani.
Amesema, “maandamano yale yasingekuwa ya amani kutokana na baadhi ya matamko yaliyotolewa na hivyo yakapewa katazo kimaandishi kwamba hayatakiwi yafanyike. Lakini Viongozi hawa waliendelea kuhamasishana na kuendelea na matamko mengine mbalimbali yenye viashiria ambavyo vilifanya Polisi iendelee na msimamo wake wa kuyakataza.”
Muliro alikuwa akitoa taarifa kwa wanahabari juu ya kukamatwa kwa watu 14, wakiwemo Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA, Mwenyekiti Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti, Tundu Lissu, Godbless Lema na Peter Lazaro ambao amesema wanaendelea kuhojiwa kwa kuzingatia misingi ya kisheria.