Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikisha wadau mbalimbali na kupendekeza namna bora zaidi ya kushughulikia suala la mmomonyoko wa maadili nchini kwa kuweka bayana wajibu wa Serikali na wa wadau wengine kwenye jamii.
Rais Samia ametoa tamko hilo leo wakati akihutubia katika sherehe za Kilele cha Tamasha la Tatu (3) la Kitaifa la Utamaduni zilizofanyika katika uwanja wa Majimaji, mjini Songea.
Aidha, Rais Dkt. Samia ametoa wito kwa kila Mtanzania kubeba jukumu la kukagua maadili katika familia yake. Vilevile, amewataka viongozi wa kimila na taasisi za kidini kwa pamoja kuungana na Serikali katika kushughulikia mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Akizungumzia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Rais Dkt. Samia amewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani ambayo imeendelea kuwa sehemu ya utamaduni wa Watanzania.
Awali, katika siku yake ya kwanza ya Ziara Rasmi Mkoani Ruvuma, Rais Dkt. Samia amekagua mradi wa ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Songea na kueleza kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo.
Kwenye ziara hiyo, Rais Dkt. Samia atakagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.