Yalikuwa ni masafa mafupi tu ya kutoka Mikocheni kuelekea Mbezi Lousi, katika usafiri nilikuwa na rafiki mpenda maandiko anaitwa Dupa Mdupange na mada kuu ya mazungumzo yetu ilikuwa ni kwanini watu wengi zama za sasa hawapendi kusoma Vitabu. Sababu zilikuwa nyingi sana lakini sote tuliziona ni nyepesi.
Dupa anasema kusoma Kitabu kunapaswa kuwa sehemu ya maisha ya Mwanadamu, licha ya kuwa anakubaliana nami kwamba Watu wengi hawapendi kusoma vitabu lakini anasisitiza kuwa kuna faida sana unaposoma Vitabu. “Sikia nikuambie Ndugu wala haina kupindapinda, yaani kama husomi Vitabu umekwisha, uko gizani na umepitwa sana na unaendelea kupitwa,” akafunga mjadala.
Kuna nukuu muhimu nilizimega kutoka kwa Mdupange …. anasema, “Fedha, majumba na magari ya kifahari si kipimo pekee cha kuyapima mafanikio ya mtu, kwani hata jambazi anaweza kupata vyote hivyo kwa njia ya ujambazi lakini Vitabu vina manufaa makubwa sana na vinasaidia kuongeza maarifa ya kuijua dunia vizuri. Asilimia kubwa ya wanaosoma vitabu wanatumia maarifa wanayoyapata kutatua Changamoto mbalimbali na wana utajiri mkubwa kuliko mtu yeyote.”
Nilikubaliana na Dupa maana niliogopa kumpinga, (hivi kwanza unapingaje kwa pointi zenye mashiko kama hizo), ingawa kiuhalisia nilitaka kuendeleza ubishi ili nipate madini zaidi na nilifanya hivyo kwa kuwa upande wake, hivyo akaja na pointi nyingine muhimu.
“Mtu ambaye hasomi Vitabu hawezi kujua faida na manufaa ya usomaji lakimni kuihalisia Kitabu ni chakula cha akili ambacho kinaimarisha uwezo wa kufikiri na kujenga hoja, kinachangamsha akili, kinaongeza maarifa, kuimarisha misamiati na hukuza uwezo wa lugha na utamkaji wa maneno kiufasaha,” alifafanua Dupa wa Mdupange.
Safari yetu na Dupa ilifikia ukingoni na tuliagana, lakini aliniachia tafakari kuu na imani kwamba ni kweli kusoma Vitabu ni njia ya kupata maarifa, kwani maarifa nijuavyo mimi ni njia inayotumiwa kujitoa katika shida ama kuweza kupata kitu, kwa kutumia elimu ama ujuzi ambao unaweza ukawa wa kuzaliwa nao au ukatokana na mang’amuzi tu ya maisha ikiwa ni pamoja na kusoma, kusikia au kutenda.
Ndugu, hapa naomba tukubaliane kwamba usomaji wa Vitabu pia huboresha kumbukumbu, yaani hujenga uwezo wa uchambuzi wa masuala mbalimbali, hujenga uwezo wa kuandika na huongeza umakini na ni njia bora ya kupunguza sononi kama ambavyo faida zaidi za usomaji wa Vitabu zinavyoonekana hapa chini baada ya kuchambua maongezi yetu na Mdupange na asikwambie Mtu, kusoma Vitabu ni muhimu sana.
Moja ya faida ya kwanza ambayo unapaswa kuielewa ni kuwa, Vitabu ni Barabara kuu ya Maarifa: Vitabu vinatoa hifadhi kubwa ya maarifa kuhusu mada yoyote inayoweza kuwaziwa. Ingia kwa kina katika Historia, Sayansi, Falsafa, hii itakusaidia kuchunguza mambo mapya ya kufurahisha na yanayokuvutia.
2. Msamiati Ulioimarishwa: Kusoma mara kwa mara vitabu, hukuweka wazi kwa anuwai ya msamiati, kuboresha ujuzi wako wa mawasiliano na ufahamu.
3. Kukuza Kumbukumbu: Tafiti zinaonyesha kwamba kusoma Vitabu kunaweza kusaidia kuboresha kumbukumbu yako na utendaji kazi na utambuzi, kuweka akili yako hai na kuhuisha maarifa kichwani.
4. Kupunguza Mfadhaiko: Ukikipenda Kitabu, inaweza kuwa njia ya kukusaidia kutoroka katika mfadhaiko, kutoa ahueni ya muda kutokana na mahangaiko ya kila siku na nafasi ya kutuliza ubongo wako.
5. Kukuza fikra: Katika ulimwengu wa kisasa wenye mwendo wa kasi uliojaa vikengeusha-fikra, kusoma Kitabu huimarisha uwezo wako wa kulenga na kukua kifikira.
6. Uelewa na Mtazamo: Kung’ang’ania usomaji wa Vitabu, kutakufanya uvae uhusika wa Mwandishi na hukuruhusu akili yako kukuza uelewa na kupata ufahamu wa kina wa mitazamo tofauti.
7. Ubunifu: Kusoma Vitabu pia hukuweka wazi kiakili na kukupa mawazo mapya ya kimichakato, ambayo inaweza kuibua ubunifu wako mwenyewe na ujuzi wa kutatua matatizo.
8. Ustadi wa Kuandika: Ukisoma Vitabu itakusaidia katika nadharia ya uandishi kwani utaboresha mtindo wako wa uandishi, muundo wa sentensi, na uwazi wa jumla wa kimawasiliano.
9. Ubora wa Kulala: Badilisha mtindo wako wa maisha kwa kupenda kusoma kitabu kabla ya kulala. Pata hali ya utulivu ya kusoma ambayo inaweza kukusaidia kupumzika na kustarehe, na kukuza ubora wa usingizi wako.
Kiufupi msomaji wa Vitabu huwa ana maudhui ya kutosha kuliko asiyesoma vitabu, na hata unapotokea ubishani au uchangiaji mada, utaona tofauti ya wasomaji na wasio wasomaji wa vitabu kwani wasio wasomaji badala ya kujadili hoja huanzisha ubishani.
Kibaya zaidi watu wasiosoma Vitabu huonesha ghadhabu, watashammbulia mtu badala ya kutetea hoja zao na mara nyingi wasomaji wa vitabu watachangia hoja kwa utulivu, kwa kujenga hoja na kutoa mifano rejea kutoka kwenye vitabu walivyosoma bila ghadhabu wala kupayuka.
MUHIMU: Wasomaji wa vitabu wanapokutana, ni kawaida yao kujadili mambo muhimu ya kujenga, lakini wasiosoma vitabu wakikosa cha kuongea huishia kuwajadili watu, hivyo nakupa siri hata ukitaka kuepukana na umbea …. jamaa yangu we Soma Kitabu.
Wasalaam.