Jeshi la Kujenga Taifa – JKT, limewataarifu Vijana watakaopata fursa hiyo kuwa Jeshi la Kujenga Taifa kuwa halitoi ajira, pia halihusiki kuwatafutia ajirakatika Asasi, Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Mashirika ya Serikali na yasiyo ya Kiserikali, bali hutoa mafunzo yatakayowasaidia Vijana kujiajiri mara baada ya kumaliza Mkataba wao.

Hayo yamebainishwa katika Taarifa ilitolewa na Kurugenzi ya Habari na Mahusiano Makao Makuu ya JKT Dodoma kwa Vyombo vya Habari hii leo Septemba 25, 2024 ikieleza kuwa pia Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Mabele, anawataarifu Vijana wa Tanzania Bara na Visiwani juu ya uwepo wa nafasi za kujiunga na mafunzo ya JKT kwa kujitolea kwa mwaka 2024.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, utaratibu wa Vijana kuomba na kuchaguliwa kujiunga na mafunzo hayo, unaratibiwa na Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambako mwombaji anaishi ambapo usaili wa kujiunga na Mafunzo utaanza Oktoba 1, 2024 kwa Mikoa yote Tanzania bara na Visiwani na watakaoteuliwa wataripoti kwenye kambini kuanzia Novemba 1-3, 2024.

Aidha, Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Mabele amewakaribisha Vijana wote watakaopata fursa hiyo ya kujiunga na Vijana wenzao, ili kujengewa Uzalendo, Umoja wa kitaifa, Ukakamavu, Kufundishwa Stadi za Kazi, Stadi za Maisha na utayari wa kulijenga na kulitumikia Taifa lao.

Rais Samia azindua jengo Ofisi ya Mkurugenzi Mbinga
Mdupange: Kama huna utamaduni wa kusoma Vitabu umekwisha