Kituo cha Kitaifa cha Uhalifu wa Mtandao cha Jeshi la Polisi nchini Nigeria, kimewakamata washukiwa watatu wanaohusishwa na kesi ya ulaghai wa ngono na kimapenzi.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi hilo, Muyiwa Adejobi ilieleza kuwa uchunguzi wa awali ulibaini kuwa washukiwa hao walikutana na raia wa Croatia, kwenye programu ya uchumba.
Ilieleza kuwa, “mazungumzo yao ya kuendelea yaliendelea hadi Instagram na WhatsApp, na kusababisha uhusiano wa karibu. Hata hivyo, Mcroatia huyo alidanganywa kutuma picha zake akiwa uchi kupitia programu ya uchumba.”
“Baadaye washukiwa hao walikula njama na kumshinikiza alipe fidia au atume picha zake kwa familia na marafiki zake kama hatafanya hivyo wakilenga kujipatia fedha isivyo halali,” alieleza Adejobi.
Washukiwa hao, ambao ni Abodunrin Rasheed, Abodunrin Tunde na Abodunrin Rokeeb walikamatwa kufuatia kutolewa kwa ripoti ya NPF-NCCC E-Reporting na ile ya kijasusi kutoka Kituo hicho.