Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ, Dkt. Mzuri Issa na Mwenyekiti wa ZPC, Abdallah Mfaume wameuarifu umma juu ya siku ya haki ya kujua, ambayo huadhimishwa kila mwaka Septemba 28, ikilenga kukuza uelewa kwa Wananchi na Wanahabari juu ya haki hiyo ambayo huchangia uwepo wa changamoto ya kupata taarifa muhimu pale wanapohoji masuala mbalimbali ya shughuli za Serikali au Taasisi za binafsi.

Kupitia taarifa yao iliyotolewa hii leo Septemba 28, 2024 imeeleza kuwa katika kuadhimisha siku ya Haki ya Kujua, wameangazia umuhimu wa haki hiyo kama chombo cha kuimarisha Demokrasia na uwajibikaji ambapo Kauli mbiu ya mwaka huu inasema, “Kuimarisha Upatikanaji wa Taarifa na Ushirikishwaji Katika Sekta za Umma.”

“Siku hii haikuja kwa bahati mbaya bali ni muhimu iliyotambuliwa na kuridhiwa na na  umoja wa mataifa chini ya tamko la haki za binaadamu la (Universal Declaration of Human Right) mwaka 1948 na tamko la umoja wa mataifa la haki za kisiasa na kiraia(ICCPR) kama ni sehemu ya uhuru wa kujieleza kwa jamii,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ, Dkt. Mzuri Issa.

Aidha, imeelezwa kuwa Haki ya kujua inahusisha uwezo wa wananchi kupata taarifa kutoka kwa serikali na taasisi za umma, hivyo kuwapa nguvu ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maamuzi yanayowagusa ambayo inachangia katika Uwazi na Uwajibikaji, Kupunguza Ufisadi, na Kukuza Ushiriki wa Raia kufahamu kuhusu masuala muhimu ya umma.

“Haki ya kujua itaongeza uwazi na uwajibikaji Serikalini, Kutambua maendeleo ya nchi yao, Kuongeza ushiriki na ushikishwaji wa wanajamii kuleta maendeleo ya nchi,” ilifafanua taarifa hiyo.

Katika muktadha huo , ZAMECO imesisitiza umuhimu wa Serikali na taasisi husika  kuzingatia sheria na kanuni zinazohakikisha upatikanaji wa taarifa na wito kwa Serikali ambao ni kuimarisha mifumo ya uwazi, kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma, na kuhamasisha jamii kuhusu haki ya kujua.

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), Abdallah Mfaume.

Wamewataka wadau wote (mashirika yasiyo ya kiserikali,  wanaharakati wa haki za binadamu, na wananchi), kuungana katika juhudi za  kuhakikisha haki ya kujua inatambulika na kuheshimiwa ambapo siyo haki tu ya msingi bali pia ni chombo cha kujenga jamii yenye usawa, uwazi, na ushirikishwaji.

“Tunatoa wito maalum wa kuzifanyia marekebisho sheria za habari hususan sheria ya Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na Sheria No.8 ya 1997 na Sheria ya Tume ya Utangazaji ya Zanzibar namba 7 ya mwaka 1997 kama ilivyorekebishwa na sheria namba 1 ya mwaka 2010,” ilifafanua taarifa hiyo.

Hata hivyo, imeatifiwa kuwa iwapo sheria hizo zitabadilishwa, Waandishi wa Habari wataweza kuzungumzia kuhusu  maendeleo na changamoto kwa uchambuzi na hivyo kuinua uwezo wa wananchi kujua zaidi masuala muhimu ya nchi.

Sehemu ya Waandishi wa Habari waliohudhuria moja ya semina mjini Unguja.

Itakumbukwa kuwa kumekuwa na harakati za kufanyiwa marekebisho sheria ya habari kwa miongo miwili, ambapo pamoja na juhudi za wadau katika hili na kupeleka maoni yao Serikalini bado suala hilo la marekebisho ya sheria za habari Zanzibar halijapatiwa ufumbuzi.

“Wakati huu tunaadhimisha siku ya haki ya kujua tunatoa wito mahasusi kwa serikali  kulingalia kwa makini na kupata sheria mpya ya habari ambayo itakidhi haki na wajibu kwa waandishi wa habari pamoja na kuwemo kipengele mahasusi kuhusu haki ya kujua na kupata taarifa,” imebainishwa.

Haya hivyo, wamesisitiza kukumbuka kuwa haki ya kujua siyo tu juu ya kupata taarifa, bali ni kujenga pia mfumo wa utawala unaowezesha Wananchi kushiriki kwa ufanisi katika maisha yao ya kijamii na kisiasa.

Picha: Rais Samia afungua kikao Maalum cha Baraza Kuu UWT Taifa
Uzalishaji Vipuri vya Migodini waanza Nchini