Wazazi Nchini, wametakiwa kujihusisha na jukumu la malezi ya Watoto, badala ya kuwaachia Walimu pekee yao kutokana na wimbi kubwa la mmonyoko wa maadili linaloikumba jamii.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu katika mahafali ya 37 ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kibakwe iliyopo Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma.
Amesema kitendo cha jumla ya wanafunzi 80 kuacha shule kati ya wanafunzi 247 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2021 kutokana na sababu za utoro na mimba, hii inaonesha kuwa kuna baadhi ya wazazi hawawajibiki ipasavyo.
” Leo jumla ya watoto 157 wanahitimu kidato cha nne huku tukiwa tumepoteza watoto 80 kutokana na tatizo la utoro na mimba za utotoni, hii sio sawa Wazazi liangalieni hili” amesisitiza Sangu.
Ameongeza kuwa, “Elimu ndiyo msingi wa kila kitu ukiamua kuwa mfanyabiashara ni lazima uwe na elimu ukitaka kuwa mjasiliamali ni lazima uwe na elimu ndo maana Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anahakikisha watoto wote wanapata elimu bila ubaguzi wowote.”
Aidha, Sangu amewataka wazazi kujiepusha na tabia ya kuwaozesha mabinti katika umri mdogo badala yake wahakikishe wanakumbatia elimu itakayowaandaa kwa ajili ya kupambana na maisha.