Abel Paul, Jeshi la Polisi – Arusha.
Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarni kwa kushirikiana na wakala wa Barabara (TANROAD), Mkoa wa Arusha katika kuhakikisha wanadhibiti ajali za barabarani wameendelea na ukaguzi wa maeneo hatarishi ambayo yanatokea ajali za mara kwa mara, ili kuchukua hatua za haraka kudhibiti ajali na kuweka alama za vidhibiti mwendo.
Akiongea katika eneo ambalo Wananchi walitoa kilio chao juu ya ajali za mara kwa mara, Mkuu wa kikosi cha usalama Barabarani Mkoa wa Arusha, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Zauda Mohamed amesema wanaangalia maeneo yenye changamoto ikiwemo la kisongo Wilayani Arumeru.
SSP Zauda ameongeza kuwa wanaendelea kutembelea maeneo yote kwa kutambua unyeti wa Mkoa huo, ambao ni kitovu cha utalii nchini kwa kukagua maeneo ambayo watalii hupenda kupita wakiambatana na wakala wa barabara, ili kufanya tathimini ya kuweka alama za Barabarani.
Aidha, ametoa wito kwa madereva na watumiaji wengine wa Barabara kuhakikisha wanafuata sheria za usalama barabarani, ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.
Mhandisi Newton Matemba kutoka ofisi ya Wakala ya Barabara Tanroads Mkoa wa Arusha ambaye anashughulika na kitengo cha Usalama Barabarani amesema wamepokea kilio cha Wananchi huku akiweka wazi kuwa maeneo yote yanafanyiwa tathimini na kuweka alama za barabarani, ili kukomesha ajali.
Naye Mwenyekiti wa kitongoji cha Ematasha Kisongo Wilaya ya Arumeru Mkoa wa Arusha, licha ya kuzishukuru mamlaka hizo kufika eneo hilo amesema kuwa eneo hilo zimekuwa zikitokea ajali eneo hilo kutokana na madereva Kwenda mwendo kasi eneo hilo akiomba vidhibiti mwendo kuwekwa kwa wakati kudhibiti changamoto hiyo.