Naibu Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde ametembelea Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), kujifunza mambo mbalimbali na kufahamiana na watumishi ikiwemo menejimenti, kwa ajili ya ushirikiano na uongozi bora.

Katika ziara hiyo, Dkt. Msonde amefanya kikao kifupi na menejimenti ya NCC, ikiongozwa na Mtendaji Mkuu, Dkt. Matiko Mturi kwenye ofisi za baraza hilo zilizopo Njedengwa, Dodoma.

Dk Msonde alilitaja Baraza la Taifa la Ujenzi kuwa ni ‘Think Tank’ ya Sekta ya Ujenzi na kusema : “Wizara inawaamini (NCC) kama chombo chake cha ufikiri (Think Tank). Hongera! Licha ya changamoto zote mlizo nazo kuanzia kutokuwepo uwiano kati ya idadi ya watumishi na majukumu 15 mliyonayo, bado mnafanya vizuri.”

Aidha, ameitaka NCC kufikiri zaidi kuhusu njia zinazoweza kutumiwa na Serikali kuwawezesha wakandarasi wazawa kutekeleza miradi mingi zaidi ya wageni kwa manufaa yao na serikali kwa ujumla.

Dkt. Msonde amesisitiza kuwa dhana zisizo na ushahidi wala ukweli kwamba wakandarasi wa ndani hawawezi, au wakipewa fedha wanazitumia vibaya au kwamba wageni ndio wanauwezo zaidi hazipaswi kushikiliwa bali kupuuzwa kwa kuwa anaamini wakiwezeshwa inavyohitajika wataweza na manufaa yataonekana.

Wakati akipendekeza kuwezeshwa zaidi kwa makandarasi wazawa kutekeleza miradi nchini, Dk Msonde ameliagiza Baraza kupitia, kuchambua na kuangalia maandiko mbalimbali yanayohusu sekta ya ujenzi kuona kama kuna vipengele vinavozuia au kusimama kama kipingamizi kwa wakandarasi wazawa kupata miradi mikubwa ya ujenzi nchini na kuitekeleza.

“Tufikiri kwa kina, nataka tuumize vichwa kuona tutawasaidiaje kwa sababu Serikali hii ya awamu ya sita chini ya mama Samia Suluhu Hassan inataka kuwatumia wakandarasi wazawa kwa kutumia rasilimali zake. Kusema tunao wengi kwa idadi kama hawatumiki kwenye miradi yao haisaidii. Serikali inataka wanufaike na vya kwao ili nayo inufaike.”

Dkt. Msonde pia amesisitiza kuhusu ushirikiano kati ya taasisi na wakala zilizo chini ya wizara ya Ujenzi akisema ushirikiano una nguvu na unasukuma taasisi kusaidiana kwa lengo la kufanikiwa kwa faida ya wote.

Kibaha: Zegezege awapa neno Wanawake Viongozi
Hekima: Ukweli unaopaswa kuufahamu maishani