Faudhia Simba, Dar24 Media – Dar es Salaam.
Wanafahamika kama Wahenga, wengine huwaita Waswahili. Walikuwa na misemo mingi sana, ambayo ina maana tofauti na ikikusudia jambo fulani ama kwa kuonya au kwa kutoa morali kwa ajili ya kufanikisha jambo husika linalomkabili mtu.
Lakini kwa leo ningependa tuuangalie huu usemao, “Kichwa kikubwa bila akili ni adhabu kwa miguu” huu ni usemi ambao bado unaishi vizazi na vizazi ukitumika au kumuhusu mtu yeyote na hata wa rika tofauti, si tu kuwa na kichwa kikubwa lakini hata miguu ambayo ni kama inayoshikilia shina na matawi kwenye mti.
Naizungumzia Timu ya soka ya Simba ya jijini Dar es Salaam, ikipewa majina mengi kutokana na umahiri wake ikiwemo lile maarufu la ‘Mnyama’ ikiwa ni moja ya Klabu bora Barani Afrika ambayo imeleta ushindani na kuuinua mpira si wa Ligi kuu nchioni pekee bali hata ukanda wa Afrika ya Mashariki ikiwa na sehemu kubwa ya mashabiki katika maeneo mbalimbali.
Ndani ya miaka minne, Mnyama alijizolea sifa kwa kutwaa ubingwa Ligi Kuu Nchini huku akifanya vizuri Kimataifa, kiasi cha kuibua furaha kwa viongozi na mashabiki wao, huku watani wao wa jadi Yanga SC wakikaa benchi kujitafuta wakisubiri zamu yao kama ilivyo kawaida katika mchezo wa soka.
Ndani ya kipindi hicho, Simba chini ya Msemaji wao Haji Manara na uongozi CEO, Barbara Gonzalenz Simba walitumia misemo mbalimbali ambayo iliwapa hofu timu pinzani kama vile Unstoppable (Haizuiliki), Do or Die (fanikisha au kufa), War in Dar (Vita Dar es Salaam) nk.
Hata hivyo, upepo ukabadilika Msimu wa 2021/22 ubingwa wa Ligi kuu Tanzania bara ukatua kwa Yanga ambao muda wote huo walisubiri huku wakitumia mbinu mbalimbali kurejea katika ubora wao hali ambayo ilileta taharuki na pengo zaidi kwani ni wakati huo huo ambao pia mhimili wao Mkuu, CEO. Barbara Gonzalenz aliachia ngazi.
Haikujulikana shida ni nini, lakini kila mmoja aliwatazama Viongozi na mashabiki walichafukwa wakawa sio wale tena ambao walikuwa na sura za nuru, lugha nzuri kwa timu na wachezaji pale wanapoizungumzia timu yao, utani kwa wapinzani wao na hata kujigamba pale ilipobidi.
Viongozi wa Simba walinyooshewa vidole vya ubaya, joto likamkumba Mwenyekiti wa Klabu hiyo Murtaza Mangungu wakitaka achie Madaraka, lakini kwa busara zake alifahamu kuwa haya ni mapito tu na alivumilia, kisha upande ukageuka kwani Mwekezaji wa Klabu hiyo Mo Dewji naye akaonja ‘joto ya jiwe’ akitakiwa kutoa maelezo ya zi wapi zilipo Bilioni 20 ambazo zinasajili Wachezaji wasio na viwango.
Maneno hayo mengi ya Mashabiki yakawa kama yanawapoteza uelekeo Viongozi Simba ambao walikuwa kila wakisajili mchezaji basi alionekana hana ubora na wao kuonekana ‘wapigaji’ mfano usajili wa Peter Chikwende, Peter Banda , Augustine Okra, Pape Sakho,Thadeo Lwanga nk. kiasi mgandamizo ulikuwa mkubwaa sana kwao.
Lakini kuna usemi usemao ‘Mvumilivu hula mbivu’ ambao uliwapa matumaini Viongozi wa Simba, kwani licha ya sajili zao kufeli lakini maneno ya faraja kwa mashabiki ikiwemo kusifia sajili toka kwa Msemaji wao Ahmed Ally ilileta matumaini, kwani aliwapamba Wachezaji na kuwarudishia mashabiki morali na umoja, hivyo walishikamana na kujenga hali ya kujiamini.
Simba ikakaza roho kwa kuachana na wachezaji wengi mahiri akiwemo Clatus Chota Chama, Henock Inonga Baka, Sadio Kanoute nk, kisha kuleta sajili za wachezaji Vijana ikiacha mshangazo kwani haikutarajiwa, ni kama walikuwa wakiunda mradi mpya chini ya kocha Fadlu Davids, hii haikuwa kazi rahisi kwake ili aweze kupata kikosi cha kwanza kwa haraka lakini dalili ya mvua ikaonekana kwa matokeo mazuri ya kimuunganiko wa timu.
Kitendo hiki cha kuachana na wachezaji mahiri na wenye majina ambao walikuwa na mchango mkubwa katika timu kiliwaumiza wanasimba lakini kadri hali ilivyoendelea walionekana kuzoea na kusahau baada ya sasa kuona sajili zao za akina Debora Fernandez, Jean Charles Ahoua, Abdulrazack Hamza, Augustine Okejepha, Leonel Ateba na wazawa kama , Awesu Awesu na wengineo.
Michezo minne ya Ligi kuu ilitosha kabisa kutoa taswira ni wapi wanaelekea, kwani yote walishinda zote bila kuruhusu goli la kufungwa, wakiwagalagaza Tabora United 3-0, Fountain Gate 4-0, Azam 2-0 na Dodoma jiji 1-0 huku wakijizolea alama 12 wakishika nafasi ya tatu nyuma ya Fountain Gate na Singida Big Star zenye alama 13 kila moja lakini zikiwa na michezo mingi zaidi.
Mwanasiasa na Mwanafalsafa, Martin Luther King aliwahi kusema, “sitamani kumjua Babu yangu alikuwa nani, ninachotaka kufahamu mjukuu wake atakuwa na tabia Gani.” Hiki ndicho walichokifanya Simba kwa msimu huu wa 2024/2025 kwani katika vita ili uachane na matumizi ya Bunduki inabidi utumie Bunduki.
Simba wasingeweza kuwa vizuri msimu huu, bila kutumia silaha ambazo ni Wachezaji wenye uwezo na wameendelea kujiboresha zaidi kwa kumsajili Elie Mpanzu ambaye atashiriki mashindano ya Kimataifa hadi pale dirisha dogo la usajili litakapo funguliwa ndipo ataanza kucheza Ligi ya ndani.
Tuna mengi ya kujifunza kupitia Simba na Yanga, lakini kwa hili la Simba linanikumbusha pia msemo wa Lucky Crackent, yeye aliwahi kusema “Muonekano siku zote hutengeneza uwezekano” japo ni ngumu na ni mapema kusema kwamba Simba msimu huu ni wao, ila jambo hili linawezekana kwani nyota njema huonekana asubuhi na dalili ya mvua ni mawingi pia.