Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt Doto Biteko amesema kuwa Serikali inathamini mchango wa viongozi wa dini wanaoeleza waumini wao kuhusu maendeleo kwa kuhimiza umoja, amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.

Dkt. Biteko ameyasema hayo katika Misa  Takatifu ya Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre wa  Dkt. Faustine Kamugisha iliyofanyika Kijiji cha Kyamulaile, Wilaya Bukoba Mkoani Kagera.

“Serikali yetu inathamini sana mchango wa viongozi wa dini wanaoelekeza watu kwenye maendeleo ili tujenge nchi ya watu wanaopendana  na kuthaminiana,” amesema  Dkt. Biteko.

Amesisitiza, “Kuwa na dini tofauti kwetu si tatizo, umoja wetu tuutunze tuendelee kukumbushana kuwa hatuna taifa lingine na mwaka huu tutakua na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa tunadi sera zetu kwa ustaarabu.”

Dkt. Biteko ametoa wito kwa waumini wa Parokia ya Minziro kuendelea kushirikiana na kumsaidia Padre Kamugisha ili afanye kazi yake ya utume vizuri “ Wakatoliki wote na sisi  sauti zetu zikawe za kumfariji Padre huyu, ziwe sauti chanya kwenye utume wake.”

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi  wa dini ikiwemo Kanisa Katoliki huku akishukuru mchango wa kanisa hilo katika huduma za jamii.

“Tunatambua na kuthamini mchango wenu katika elimu kwa kutoa elimu bora na shule za kanisa hili zimekuwa zikifanya vizuri na kwa upande wa hospitali mfano Hospitali ya Kagondo imekuwa ikitoa huduma bora kwa wananchi, imetupa chachu na sisi kuboresha hospitali yetu,” amesema Mwassa.

Askofu Mkuu wa Jimbo la Bukoba, Jovitus Mwijage amempongeza Padre Faustine Kamugisha kwa kutimiza miaka 25 ya upadre na kusema kuwa Padre huyo amekuwa na juhudi katika kufanya utume wake na kujiendeleza katika masuala mbalimbali.

Wahimizwa kuhamasisha uanzishwaji Vituo vya kulea Watoto
Habarikuu kwenye Magazeti ya leo Oktoba 5, 2024