Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike duniani, wadau wa michezo kwa maendeleo Zanzibar wameandaa shughuli mbalimbali za michezo kwa maendeleo (S4D), zenye lengo la kuhamasisha ushiriki wa watoto wa kike na usawa wa kijinsia katika michezo.

Wadau hao ambao ni Jumuiya ya wanasheria wanawake Zanzibar (ZAFELA), Kituo cha mijadala kwa vijana (CYD) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) wamesema wanaamini maadhimisho hayo yanalenga kuinua ari ya watoto wa kike kushiriki kwenye michezo, kupinga ukatili wa kijinsia, na kuboresha usawa wa kijinsia visiwani Zanzibar.

Kupitia taarifa iliyotolewa kwa Vyombo vya Habari na Wadau hao imeeleza kuwa, maadhimisho hayo yatashirikisha wanafunzi kutoka skuli za Unguja katika wilaya ya Kaskazini ‘A’, Mjini, Kati na magharibi ‘A’, na yataanza kwa shamrashamra za mechi za Mpira wa pete (Netball) za kirafiki, zitakazohusisha timu za watoto wa kike kutoka skuli za Tumbatu, Jongowe, Mkokotoni, Mto wa Pwani, Kianga, Mtoni, Kiembe Samaki “B” na Uroa.

Shughuli nyengine zitakazofanyika ni ziara kwenye skuli mbalimbali na kuendesha michezo kwa maendeleo (S4D) ambayo itawafundisha wanafunzi namna ya kujikinga dhidi ya ukatili wa kijinsia, pamoja na kuwaelimisha kuhusu masuala ya wanawake na uongozi.

Aidha, taarifa yao imefafanua kwa pia Wanafunzi watashiriki kwenye uchoraji wa picha ambazo zitaakisi maudhui ya S4D na kuwapa fursa ya kuelezea mawazo yao kuhusu michezo na usawa wa kijinsia.

Kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika siku ya Jumamosi tarehe 12 Oktoba, 2024 ambapo itachezwa mechi ya fainali ya Mpira wa pete (Netball) na pia picha zilizochorwa na wanafunzi zitaoneshwa.

 

Taarifa hiyo pia imearifu kuwa Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto, Anna Athanas Paul ambaye ataongoza shughuli ya kukabidhi zawadi kwa washiriki.

Wadau hao pia wamefafanua kuwa wanaamini kuwa maadhimisho hayo ni sehemu ya mkakati wa wadau wa S4D Zanzibar wa kuendeleza usawa wa kijinsia na haki za mtoto wa kike kupitia michezo.

Picha: Matukio ya utangulizi #Knockoutyamama
Dkt. Mzuri: Waandishi mripoti Habari za Tabianchi