Johansen Buberwa – Kagera.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajjat Fatma Mwassa ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kutumia fursa inayotolewa na Serikali ya upatikanaji wa elimu ya watu wazima na nje ya mfumo rasmi, ili kujiendeleza na kuitaka idara ya elimu mkoa huo kuona fahari ya uwepo wa idadi nyingi ya vyuo na vituo vinavyotoa elimu ya watu wazima kutumika kuondoa idadi ya watu wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu kutoka asilimia 3.3 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.

Akizungumza katika maadhimisho ya kilele juma la elimu ya watu wazima kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Afisa elimu Mkoa, Michael Ligola amesema maadhimisho hayo ni utekelezaji wa sera ya elimu na Serikali ambayo imedhamiria kutimiza azima ya kuwa na watu walioelimika kutokana na kauli mbiu ya wiki ya elimu ya watu wazima mwaka huu inayosema ujumuishi katika elimu bila ukomo kwa ujuzi,ustaimilivu amani na Maendeleo.

Amesema, “katika dira ya Taifa ya maendeleo ya mwaka 1925 na malengo endelevu ya dunia (SDG) ambapo moja ya lengo la dira ya mwaka 2025 ni kuhakikisha kuwa Tanzania ifikapo 2025 inakuwa na watu waliosoma na jamii iliyoelimika sambamba malengo endelevu ya dunia yanayosema elimu kwa wote ifikapo 2030.”

Ligola amesema, eneo la elimu ya watu wazima na nje ya mfumo rasmi inajumuisha makundi matano moja ni mpango wa elimu ya msingi kwa waliokosa (MEMKWA), mbili ni mpango wa elimu ya sekondari kwa waliokosa (MESKWA) , tatu ni Mpango wa uwiano elimu watu wazima na jamii (MUKEJA) nne ni mpango wa elimu kwa njia mbadala unajumusha mradi wa kuboresha elimu ya sekondari kwa watoto wa kike (SEQUIP) na tano ni Elimu ya ufundi.

Kwa upande wake Afisa elimu ya Watu wazima na nje ya mfumo rasmi na elimu maalum mkoa wa Kagera, Fortunatus Kahwa amesema idara ya elimu na wadau wanaendelea kushirikiana kwa kuhakikisha changamoto ya uwepo watu wazima 4184 mkoni humo kuanzia miaka 19 na kuendelea wasiojua kusoma, kuandika pamoja na kuhesabu inafanyiwa kazi.

Aidha, ameyataja mafanikio ya sasa kupitia kutekelezwa kwa mpango huo kuwa ni Wanafunzi 5,436 kati ya 6,723 sawa na asilimia 81 wa MEMKWA waliofanya mtihani wa kitaifa mwaka 2023 wa upimaji darasa la saba wamefanikiwa kujiunga na mfumo rasmi.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Dar24 Media Mkoani Kagera akiwemo Nicolaus Martin na Sadam Abdallah wamesema, jamii bado haijapata elimu ya kutosha namna ya kuipata hiyo elimu na kuiomba Serikali iongeze miundombinu ya kutosha pamoja na muda maalumu kwa watakaopata elimu hiyo.

Hatimaye Boniface Jacob apatiwa Dhamana