Lydia Mollel – Morogoro.

Wazazi na walezi wametahadharishwa kuacha matumizi holela ya dawa, ili kuepuka tatizo la usugu wa vimelea vya dawa, hasa kwa wale wenye tabia ya kutomaliza au kutumia dawa bila uchunguzi wa kitabibu .

Tahadhari hiyo imetolewa na Mkuu wa Chuo cha Afya Hermargs Mipango na Fedha, Oljein Kikoti wakati wa maadhimisho ya Siku ya Watoto Wenye Utindio wa Ubongo Duniani, walipotembelea kituo cha kulelea watoto cha Erick Memorial Foundation, ambapo lengo lilikuwa kutoa elimu kwa walezi wa kituo hicho juu ya matumizi sahihi ya dawa.

Amesema, “usugu wa vimelea vya Magonjwa Dhidi ya Dawa ni ile hali ya bacteria wanaosababisha magonjwa kuwa na uwezo mkubwa zaidi ya dawa zinazotumika kutibu magonjwa kwenye mwili wa binadamu na hii inatokana na matumizi holela ya dawa kwa kutokufata taratibu au ushauri wa kitaalamu.”

Kikoti, amesema lengo la kutoa elimu hiyo ni kuwajengea uwezo walezi wa watoto wenye ulemavu, kwa kuwa watoto hao hawana uwezo wa kujihudumia wenyewe. Hii itawasaidia walezi kufuata taratibu sahihi za kuboresha huduma za afya na kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa madaktari.

Naye Mfamasia Pascal Mollel amewahimiza wazazi na walezi kuepuka imani za kishirikina, zinazowaminisha kuwa mtoto mwenye utindio wa ubongo amerogwa,badala yake, amewashauri kufika katika vituo vya afya ili wapate vipimo na ushauri sahihi kutoka kwa wahudumu wa afya.

Veronica John, Mlezi wa Kituo cha Erick Memorial Foundation kinachowalea watoto wenye utindio wa ubongo, amesema elimu waliyopata itawawezesha kuwahudumia watoto hao vizuri zaidi.

Ameongeza kuwa wamepata uelewa juu ya madhara ya matumizi holela ya dawa, jambo ambalo hawakulitambua awali, na sasa watakuwa makini zaidi wanapowapatia watoto dawa lakini pia anaiomba serikali na jamii kujitokeza kuwasaidia, ili waweze kupata miradi itakayowasaidia kuendesha kituo hicho pamoja na kuwalipa watoa huduma.

Arusha: Wawili wadakwa kwa mauaji ya Israel
Maadhimisho siku ya Mbolea: Sendiga awaita Wananchi Babati