Faudhia Simba, Dar24 Media – Dar es Salaam.

Ni kiungo wa kati, lakini anaweza cheza kama winga wa kushoto, kiungo mkabaji, kiungo wa kujihami na kama mchezaji anayecheza kwa kusogea mbele kupeleka mashambulizi akitokea nyuma, akifuata nyayo za kaka zake wawili ambao ni mapacha wakicheza mpira wa miguu wa timu ya taifa ya Guinea.

Alizaliwa Machi 1993 na kulelewa katika jamii ya mashariki mwa Paris ya Lagny-sur-Marne, ambapo katika ukuaji wake na maisha ya kielimu yeye alikuwa ni mwanafunzi mwenye nidhamu aliyefanya bidii shuleni, lakini hamu yake kuu ilikuwa ni kucheza soka, hii ilimkaa kwenye damu.

Muda wa likizo au ambao hakukuwa na masomo, alipendelea kwenda katika uwanja wa City Stade mwendo wa saa saba kutoka nyumbani kwao ili tu kuhakikisha amelisakata soka na hata hivyo baadaye wazazi wake walitengana lakini walihakikisha wanatimiza jukumu kubwa katika ukuwaji wake wa kisoka.

Hii ilitokana na hamu kubwa ya mchezo huo wa Mtoto wao na hata wakati alipojiunga na klabu yake ya kwanza Roissy-en-Brie, iliyokuwa maili chache kutoka nyumbani kwao, wala hawakushangaa kutokana na sifa au umahiri wake katika mchezo huo tangu akiwa mdogo.

Alijiunga na Klabu ya Roissy akiwa na umri wa miaka sita na kuanza maisha katika klabu hiyo kama mshambuliaji, wakati ambao tayari alikuwa ameweza kuonesha umahiri wake na nidhamu suala ambalo lilimsaidia kufanikisha uvukaji wa changamoto na kufikia sehemu fulani ya mafanikio kisoka, akihudumu hapo kwa miaka sita kabla ya kujiunga na Us Torcy.

Namzungumzia Paul Labile Pogba, Mfaransa mwenye asili ya Guinea aliyewahi pia kuwa nahodha wa timu ya watoto chini ya umri wa miaka 13 na baada ya msimu mmoja kuisha akiwa klabu ya Torcy, Pogba alijiunga na klabu ya wataalamu ya Le Havre.

Katika msimu wake wa pili katika klabu hiyo, Pogba alikuwa nahodha katika timu na kuifikisha timu yake hadi fainali, Championnat National ya watoto wenye umri chini ya miaka 16 ikaipa ushindi timu ya Pogba ijulikanayo kama Le Havre na timu ya Pogba ikawa ya kimataifa kwa kupata ushindi.

Baada ya kuhamia Manchester United miaka miwili baadaye, mechi chache zilitosha kuonesha ufundi wake na ndipo alijiunga na Juventus ya Italia kwa uhamisho wa bure mwaka 2012 na kuisaidia klabu hiyo kutwaa mataji manne mfululizo ya Serie A, mawili ya Coppa Italia na mawili ya Supercoppa Italiana.

Wakati akiwa nchini Italia, Pogba alidhihirisha kuwa mmoja wa wachezaji chipukizi wenye kutegemewa zaidi duniani kwa kupokea tuzo ya Golden Boy mwaka 2013, ikifuatiwa na Tuzo ya Bravo mwaka 2014, ambapo mwaka 2016 aliitwa kwenye Timu ya mwaka ya UEFA 2015 na 2015 FIFA FIFPro World XI baada ya kuisaidia Juventus kufika Fainali ya Ligi ya mabingwa ya UEFA 2015, ikiwa ni fainali yao ya kwanza katika kipindi cha miaka 12.

 

Uchezaji wa Pogba akiwa Juventus ulimfanya arejee Manchester United F.C. mwaka wa 2016 kwa ada ya uhamisho wa rekodi ya dunia wakati huo ya pauni 105 milioni ikiwa ndiyo ada iliyokuwa ya juu zaidi kulipwa na klabu ya Uingereza hadi mwaka 2021 na katika msimu wake wa kwanza alishinda Kombe la Ligi na Ligi ya Europa.

Kimataifa, Pogba aliongoza Ufaransa kwa ushindi katika Kombe la Dunia la FIFA la U-20 2013 na kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora kwa uchezaji wake wakati wa mashindano, akianza rasmi sasa kuichezea timu ya waandamizi mwaka mmoja baadaye na kushiriki vyema katika Kombe la Dunia la FIFA la 2014.

Akaja kutunukiwa Tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi na baadaye aliwakilisha taifa lake kwenye UEFA Euro 2016 katika ardhi ya nyumbani kwao Ufaransa, ambapo walimaliza kama washindi wa pili, kabla ya kushinda Kombe la Dunia la FIFA la 2018, akifunga katika fainali.

Adui mkubwa wa mchezaji huyu ni majeraha, pamoja na uhodari wote huo lakini hajawahi hata kuigusia ballon D’or na hata alipokuwa Manchester united aliwahi kukosa zaidi ya michezo 100 na kupata kwake majeraha ya mara kwa mara harafu akirudi kwenye pichi anakuwa na kasi ile ile kulileta maswali mengi, hasa katika kipindi ambacho alikabiliwa na kesi akiendelea kutumikia adhabu.

Anatuhumiwa kwamba miaka yote kuwa amekuwa akidanganya uwezo wake hii na hii ilibainika katika ufunguzi wa msimu pale alipofanyiwa kipimo na kupatikana viwango vya juu vya testosterone mwilini na kupelekea Mahakama ya kupambana na dawa za kusisimua misuli huko nchini italia (NADO), kuthibitisha kusimamishwa kwa mchezaji huyo ndani ya miaka minne, kufuatia hukumu ya kesi iliyosomwa Agost 20, 2023.

Kifungo cha miaka minne kwa mchezaji huyu ni kama kumtoa kwenye dira, kwani licha ya majeraha lakini pia tunaongelea mwaka 2027 ndipo atakuwa huru wakati ambao tayari atakuwa amefikisha miaka 34 na hata akirejea atakuwa hana timu na kwa umri wake huenda asiweze kucheza tena, kitu ambacho kilimfanya kukata rufaa kwani kuna mengi hakuyasema kipindi kesi inasomwa kwamba alipewa virutubisho vya chakula na rafiki yake ambaye ni Daktari huko Miami, bila kujua kilichomo ndani.

Alilaumiwa kwa kutosema ama kuwashirikisha madaktari wa klabu yake ya Sasa ambayo ni Juventus na kusababisha kukosa msaada au kupata usaidizi hafifu katika kesi yake, lakini rufaa yake imempa matumaini mapya ya kurejea kwenye soka kwani miezi 48 ya adhabu yake sawa na miaka minne, sasa imekuwa ni miezi 18 na hivyo atarejea uwanjani Machi 2025, baada ya Mahakama ya usuluhishaji wa michezo CAS kukiri kuwa mchezaji huyo akitumia dawa hizo bila kujua.

Paul Pogba mchezaji wa Juventus ambayo inashiriki ligi ya Seria A Nchini Italia, amekuwa na msimu mzuri tangu alipojiunga na miamba hiyo akishinda taji la Seria A ndani ya misimu yake minne ya kwanza na ubora wake ndio ulichangia Juventus kutaka huduma yake lakini kwasasa ataendelea kutumikia adhabu yake hadi hapo mwakani 2025.

Hata hivyo, hatua hii bado inawaumiza kichwa Viongozi wa Juventus ambao wanatamani kupunguza mshahara wa Pogba, huku wakitafakari juu ya majeraha yake ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakifanya mchango wake kuwa mdogo katika timu.

Tukio la Paul Pogba linatupa funzo kwamba siku zote usimuamini mtu hata kama ni nani rafiki yako. Kuwapa nafasi ya kuwaamini watu, ndicho chanzo cha Pogba kutumia supriment ambayo ni aina ya vyakula vya kuongeza nguvu katika mfumo wa madawa na kuleta sakata lote hili ambalo bila shaka utakubaliana nami kuwa lina mtikisoko katika maisha yake kisoka.

Kunguru mwoga hukimbiza mbawa zake. Ni msemo wa wahenga una maana kubwa sana kwani cheche siku zote huzaa moto, yaani namaanisha kuwa kitu kidogo huweza kuleta madhara makubwa, hivyo ni vyema kuwatahadharisha watu wanaodharau mambo madogo kwani huweza kusababisha madhara makubwa yasiyotegemewa kama ilivyomtokea Paul Pogba. Chunga sana marafiki, ili UBAYA usikufanikishie UBWELA kwenye ‘mishe’ zako.

Uchaguzi Serikali za Mitaa: Toima awapa neno Wananchi Manyara
Maafisa Elimu acheni kuzalisha madeni - RC Mwasa