Abel Paul, Jeshi la Polisi – Arusha.
Polisi Mkoani Arusha, imefafanua taarifa iliyoyolewa na baadhi ya Vyombo vya Habari kuwa kwenye nyumba ambayo ulikutwa mwili wa mtoto Mariam Juma, aliyeuawa Oktoba 12, 2024 kwa Mrombo, kulikutwa risiti za malipo ya vifo au mauaji yaliyofanyika kishirikina habari ambazo si za kweli.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandimizi wa Polisi Justine Masejo amesema wamefuatilia na kubaini kuwa Baba mwenye nyumba, Ramji Mlacha, Kiongozi wa Chama cha Wapare washio Arusha, alielekeza kwamba mmoja wao akipatwa na msiba kila mwanachama huchanga na nakala hubaki kwa mchangishaji.
Amesema, risiti zilizokutwa kwenye nyumba hiyo kwa mujibu wa ushahidi uliopatikana si risiti za vifo vilivyotokana na ushirikina kama baadhi ya watu na baadhi ya vyombo vya habari vinavyoendelea kupotosha umma.
Kamanda Masejo amesema nguo mbalimbali ikiwepo masweta imebainika ni ya watoto na wajukuu waliokuwa wakiishi katika nyumba hiyo, huku ikitoa onyo kwa baadhi ya watu wanaoendekeza tabia za kuzusha mambo ya uongo bila kuwa na uhakika kutoka mamlaka zinazostahili kuacha tabia hiyo.
Aidha, amekemea tabia iliyooneshwa na baadhi ya watu waliojichukulia sheria mkononi kwa kufanya uharibifu katika nyumba ya mtuhumiwa huyo wa mauaji, wakati hatua stahiki zilisha huchukuliwa kwa haraka na kwa wakati, ikiwemo kuwakamata watuhumiwa.