Bunge la Seneti nchini Kenya, likiongozwa na Spika Amason Kingi limemuondoa madarakani Naibu Rais wa nchi hiyo Rigathi Gachagua, kufuatia zoezi la siku mbili za kuwasilisha hoja na kuzifafanua, ambapo alikutwa na hatia ya mashtaka matano kati ya 11 yaliyomkabili.
Gachagua, ambaye amelazwa katika Hospitali ya Karen jijini Nirobi, ameondolewa madarakani baada ya maseneta 53 kupiga kura kuunga mkono shitaka la kwanza la ukiukaji wa vifungu namba 10, 27, 73, 75, 129 vya Katiba ya Kenya.
Awali, Maseneta 13 pekee ndio waliopiga kura kupinga shitaka hilo kama ilivyobainishwa katika hoja ya kumuondoa madarakani iliyowasilishwa na Mbunge wa Kibwezi, Mwengi Mutuse.
Kabla ya kura kupigwa, Mawakili wa Rigathi Gachagua waliomba kikao kiahirishwe ambapo Wakili Kiongozi, Paul Muite aliwataka Maseneti hao kuwapa muda hadi Oktoba 22, 2024 ili mteja wao aweze kujitetea mbele yao, lakini waliondoka baada ya Maseneta kuridhia mchakato uendelee.
Kuhusu afya ya Gachagua, Tabibu Mkuu Dkt. Dan Gikonyo alisema alipata maumivu makali ya kifua na ikamlazimu alazwe na ataendelea kuwa chini ya uangalizi kwa saa 72 zijazo na inaarifiwa kuwa ilikuwa ni haki yake kujitetea mbele ya baraza , lakini Maseneta hao waliridhia kuendelea na mchakato bila uwepo wake.
Mbali na mashtaka ya kujilimbikia mali kwa njia zisizo za halali, Gachagua alituhumiwa pia kwa kutumia watu wa kando kujipatia kandarasi ya vyandarua vya mbu vilivyotiwa dawa vya thamani ya shilingi bilioni 3.7, kupitia Mamlaka ya Ununuzi wa Bidhaa za Tiba, KEMSA.
Kuhusu utaratibu unaofuata, ni kumteua mrithi wa Naibu wa Rais atakayehitaji ridhaa ya Bunge la Taifa na Rigathi Gachagua anayo fursa ya kufika Mahakamani, ili kulisafisha jina lake na kuweza kubatilishwa kwa uamuzi huo ingawa kikatiba uamuzi uliopitishwa umemfungia milango ya kuwania nafasi ya uongozi wa umma.