Rais wa Kenya William Ruto amempendekeza Waziri wa usalama wa ndani wa Taifa hilo, Kithure Kindiki kuchukua nafasi ya aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ambaye ameondolewa madarakani na Bunge la Seneti.
Taarifa ya Kindiki imethibitishwa na Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetangula wakati wa kikao maalum cha hii leo asubuhi Oktoba 18, 2024 ambapo alikuwa ni miongoni mwa majina yaliokuwa yamependekezwa kuchukua nafasi hiyo ya Umakamu wa Rais.
Rigathi Gachagua (59), anakuwa Naibu wa kwanza wa Rais kuondolewa katika nafasi hiyo kufuatia utaratibu ambao haujawahi kushuhudiwa na kumaliza mzozo wa miezi kadhaa, kati yake na Rais William Ruto akishutumiwa kwa ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka.
Ruto alikuwa na siku 14 za kupendekeza jina la Naibu wake mpya baada ya kuondolewa kwa Gachagua, lakini hatua yake hiyo sasa inatoa nafasi kwa Bunge la Kitaifa ndani ya muda wa siku 60 kwa kutumia Katiba ya Taifa hilo kujadili na kuidhinisha jina la Kindiki kuhudumu katika wadhifa huo.