Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema Tanzania na Singapore zitaenzi uhusiano uliopo kati yao ambao umedumu kwa muda mrefu, ikiwemo kuongeza ufanisi katika ufanyaji wa biashara.

Dkt. Biteko ameyasema hayo akiwa nchini Singapore mara baada ya kukutana na kufanya mazungunzo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Singapore Mhe. Gan Kim Yong.

Amesema, “tunatakiwa kujifunza kutokana na uhusiano huu na hasa kutoka Singapore kwa kuwa mmepiga hatua katika sekta ya nishati hadi kuwa na uwezo wa kufikia mahitaji ya juu ya umeme ya zaidi ya Gigawati 8, hicho ni kiasi kikubwa ikilinganishwa na Tanzania yenye takribani Megawati 3000 ambapo hadi mwaka 2030 tumepanga kufikia Megawati 10,000.”

Aidha, Dkt. Biteko ameipongeza Singapore kwa uzalishaji wa umeme wa jua na kusema kuwa Tanzania inaendelea na jitihada zake za kuzalisha umeme huo na kutaja miradi ya nishati inayoendelea kutekelezwa, akisema kwa sasa nchi inaendelea na utekelezaji wa mradi Julius Nyerere (JNHPP)utakaozalisha megawati 2115.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu wa Singapore, Yong amesema nchi yake ipo tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania na kuwa nchi hizo zina mahitaji ya kufanana na kwamba Singapore hutumia zaidi gesi asilia kama chanzo cha nishati ingawa pia inatumia umeme unaozalishwa kwa maji, jua na upepo.

Maisha: Amuokoa mkewe asipasuliwe wakati wa kujifungua
DC Faiza awahimiza Wanabusega matumizi Nishati Safi