Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameonesha kutoridhishwa na usimamizi na kasi ya ujenzi wa Barabara ya Nyamwage – Utete (km 33.7) kwa kiwango cha lami na kumuagiza Meneja wa Wakala ya Barabara (TANROADS) Mkoa wa Pwani, Eng. Baraka Mwambage kumsimamia Mkandarasi China Railway Seventh Group (CRSG) akamilishe kuleta Wataalam pamoja na Mitambo itakayomwezesha kutekeleza mradi kwa wakati na kwa mujibu wa mkataba.

Bashungwa ametoa agizo hilo leo Oktoba 24, 2024 Wilayani Rufiji Mkoani Pwani wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo na kutoridhishwa na utendaji kazi wa Mkandarasi huyo ambapo hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 7.

Amesema, “Meneja wa TANROADS hakikisha unamsimamia Mkandarasi kama mikataba inavyosema, nitarudi hapa kukagua nataka nione timu yote ya wataalam wakiwa wamejipanga pamoja na vifaa vya kazi vikiwa site, hiyo siku ukiwa hujasimamia haya narudi na wewe Dodoma.”

Aidha, Bashungwa amemtaka Mkandarasi CRSG kujitathimini katika miradi yote anayoitekeleza kwa kuwa amekuwa akisua sua katika baadhi ya miradi ya ujenzi wa barabara ikiwa ni pamoja katika Mikoa ya Mara, Katavi, Ruvuma, Dar es Salaam na Pwani huku akitoa wito kwa Wananchi kutoa ushirikiano wakati wa utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema kuwa Rais Dkt. Samia ameidhinisha kuanza kwa maandalizi ya ujenzi wa barabara mpya km 354 inayotoka Chalinze – Magindu- Bwawa la Mwalimu Nyerere – Utete.

Naye, Meneja wa TANROADS, mkoa wa Pwani Eng. Baraka Mwambage ameahidi kumsimamia mkandarasi huyo ili aweze kuongeza kasi ya kufanya kazi wastani wa asilimia 8 kwa mwezi ambapo sasa anafanya kazi wastani wa asilimia 2.1 kwa mwezi.

Hon. Londo Sworn in as Ex-Officio Member of EALA in Kampala
Samia Kalamu Awards: TAMWA waongeza muda uwasilishaji kazi