Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew, amelieleza bunge kuwa utekelezaji wa Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria wa Igaga, Mwamashele na Lagana kwa mujibu wa mkataba umekamilika.
Ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma wakati akijIbu swali la Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo, aliyehoji lini Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria wa Igaga, Mwamashele na Lagana wenye thamani ya Tshs. Bilioni 6.6 utakamilika.
Mhandisi Kundo amesema kazi zilizofanyika katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa bomba kuu umbali wa Kilomita 33.65, Ujenzi wa Tangi la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 100,000 katika Kijiji cha Lagana.
“Ujenzi wa vituo sita (6) vya kuchotea maji katika Kijiji cha Lagana na Ulazaji wa bomba la usambazaji maji umbali wa Kilomita 7.86 katika Kijiji cha Lagana ikijumuisha matoleo ya maji (Offtake) sita (6) katika vijiji vya Igaga, Isagala, Mwamashele, Busongo/Mwamanota, Bubinza na Mwamadulu,” amesema Mhandisi Kundo
Amesema Katika vijiji vya Mwamashele na Mwamadulu Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria wa Igaga, Mwamashele na Lagana unatoa huduma kwa wananchi wapatao 3,040 wa Kijiji cha Lagana.