Na Heldina Mwingira, Dar24 Media – Dar es Salaam.

Ni tabia ya mzazi mmoja kulea Mtoto peke yake, au kwa lugha rahisi twaweza kusema utamaduni wa Watoto kulelewa na mzazi mmoja unazidi kushika kasi nchini na hata duniani kiujumla.

Kiuhalisia lipo ongezeko kubwa la watoto wanaolelewa ama kukuzwa na mzazi mmoja, tofauti na mila na tamaduni za miaka ya nyuma na kwasasa suala hili linaonekana kuwa ni la kawaida ingawa kiuhalisia Wazazi wengi hasa upande wa kike wamekuwa wakiumia kutokana na uhalisia.

Aidha, utafiti pia unaonesha kuwa waathirika wakubwa wa kulea watoto peke yao ni Wanawake ambao hutengeneza asilimia 88 ya wazazi wanaolea watoto bila msaada wa wenzi wao wa jinsia ya kiume.

Ukweli ni kwamba idadi ya familia zinazoishi na mzazi mmoja inaongezeka, hasa katika maeneo ya mijini na tabia hii kiukweli imeendelea kushamiri sababu zikitajwa kuwa wazazi kutengana, kutoelewana, kufarakana, au kutokea kifo cha mmoja wao nk.

Umoja wa Mataifa, kupitia machapisho yake kadhaa imewahi kunukuliwa ikieleza kuwa nchi za China, Iran, India, Indonesia, Israel, Jordan na Uturuki, ndizo zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto wanaoelelwa na mzazi mmoja.

Hii ina maana kuwa kwa wastani zaidi ya asimilia 10 ya watoto katika mataifa hayo, wanalelewa na mzazi mmoja, idadi ambayo ni theluthi moja ya familia za aina hii duniani kwa nchi hizo.

Nchini Afrika Kusini, inakadiriwa kuwa karibu asilimia 40 ya watoto wanaishi na mama pekee, wakati ni asilimia 4 tu wanaoishi na baba pekee huku Kenya ikikadiriwa kuwa na asilimia 30, na Msumbiji asilimia 36 kwa takwimu za nyuma kidogo.

Kiuhalisia utamaduni wa Watoto kulelewa na mzazi mmoja unazidi kushika kasi si huko bali hata hapa kwetu nchini Tanzania na ndiyo maana Dar24 Media imemtafuta Rita Paul ambaye naye amekumbwa na changamoto ya kulea mtoto peke yake kwa kutaka kujua adha gani alizipitia.

Yeye anasema, “kulea mtoto bila baba ni changamoto mno baada ya kugundua mimi ni mjamzito, mwenye mzigo kanikataa mbaya zaidi nilikuwa sina kazi wala biashara yeyote nilipaata msongo wa mawazo na baada ya kujifungua nilipata changamoto katika kulea na kuna muda anahitaji nimuoneshe baba yake.”

Licha ya wengi wao kuhalalisha aina hii ya uleaji, lakini Wanasaikolojia wanasema hakuna mtoto anayetamani kukuzwa au kulelewa na mzazi mmoja na kitendo hicho kina athari kwa watoto waliolelewa na mzazi mmoja ambazo watakuja kukabiliana nazo baadaye katika maisha yao.

Mahojiano yetu yakahamia kwa Nuru Nchimbi ambaye yeye alionekana kujisifia na wala hajutii kulea mtoto peke yake akisema nalidhamiria kuzaa na kulea peke yake kwani hataki kuendeshwa na Mwanaume.

“Na  wala sijutii ‘as long as’ naishi na mwanangu anasoma na anaishi maisha mazuri sijawahi kumfikiria baba yake hata siku moja,’ anafafanua Nuru kwa bashasha.

Maelezo haya yanatosha kuonesha kuwa hali hii imezoeleka na kiuhalisia inaonesha uwepo wa wimbi la Wanawake wanaotaka kulea watoto wao bila msaada wa wanaume na ndiyo maana wengi wao hufanya maamuzi ya kubeba ujauzito na kukataa kuendelea na mahusiano ya kimapenzi na muhusika.

Kuna ambao humficha baba wa mtoto asijue kwamba huyo ni mwanae na wengine huamua kubeba ujauzito wa mume wa mtu wakijua fika kuwa mhusika atakataa malezi kwa kujiepusha na mtafaruku unaoweza kumtokea katika ndoa yake hivyo kuwa rahisi kwao kufanikisha malengo yao.

Mwanasaikolojia, mchambuzi wa mambo ya kijamii, Justus August anasema tabia hii haikuzoeleka kiasili toka awali ila huenda imesababishwa na mabadiliko ya majukumu kwani kwasasa Wanawake nao wanajishughulisha katika utafutaji tofauti na zamani.

Anasema, “Dunia imekuwa na mentality ya kuwa mimi nitazaa au nitazalisha tu ila mtoto nitamchukua na kumlea peke yangu. Watu wanadanganyana kuwa kuishi kwenye ndoa sio kitu cha maana bali mtu anaona kawaida kuwa na Watoto ili kubaki huru na kutowajibika kwa mtu yeyote.”

Huenda inawezekana kuwa yapo mambo chanya ambayo mtu hujifunza kwa kutunza mtoto au watoto peke yake ikiwemo kugundua uwezo alionao katika kulea na kukaa na watoto, tofauti na dhana ya kuwa na uleaji wa wazazi wawili, lakini hiyo haiondoi ukweli kuwa Mtoto ana uhitaji wa pande mbili za malezi.

August anasema zipo athari kwa mtoto kwani anaweza kukosa usawa wa malezi hivyo hupelekea kushindwa kuchangamana na jinsia nyingine, kutoona umuhimu wa kuwa kwenye ndoa hivyo uharibifu unaendelea.

Sababu nyingine ni kuongezeka kwa watoto ambao hawawajibiki na kutafuta mtu wa kumpa lawama na visingizio unakuta mtu mpaka miaka 20 bado anatafuta utambulisho kuwa baba yake yuko wapi hii huleta athari.

Anashauri namna ya kupunguza changamoto hiyo katika jamii yetu kwa kuhakikisha wazazi wasiwe sehemu ya kumnyima mtoto haki yake kwa kuzuia mimba zisizopangwa na kuimarika upendo baina tao.

Pia anasema watu maarufu wanaweza kutumika katika kuelimisha jamii kwa kupiga kelele, kuimba nyimbo na kufanya kampeni zinazohusu umuhimu wa malezi wa wazazi wawili na serikali kuweka elimu ya malezi katika mitaala kwa kufundisha kuanzia shule za msingi.

“Watoto waliolelewa na mzazi mmoja, na hasa mama peke yake, huharibika, wawe wa kiume au wa kike, kwa sababu akina mama single wengi hujawa na hisia za kupungukiwa kupenda au kupendwa. Sasa, kwa kuwa yeye yuko peke yake, bila mume, hujijengea hisia mpya, za kupenda zaidi na hisia hizo huhamishiwa kwa mtoto. Yaani anaamua ‘kumhonga’ mtoto mapenzi ambayo yalipaswa kuelekezwa kwa baba yake na kwa kufanya hivyo anamharibu mtoto,” alibainisha.

Inaarifiwa pia watoto ambao huishi na kulelewa na mzazi mmoja wapo katika hatari ya kutenda uhalifu wa makosa ya jinai na katika kutafuta ukweli, Dar24 Media ilifanikiwa kumuhoji wakili Denisia Michael, ili aeleze uhalisia wa jambo hili.

“Hayo ni maneno ya mtaani tu ila hamna mahusiano yoyote kati ya kutenda kosa mna malezi hajawahi kuona utafiti kuhusiana na hilo akasisitiza kuwa mtu yeyote anaweza akatenda kosa hata kama ana wazazi wote wawili,” anakataa Wakili Denisia.

Nilifanikiwa pia kuongea na Arima Yamsaka yeye aliishi na mama yake na kusema kuwa aliathirika kisaikolojia na kuna muda alitamani ajue ladha ya kuwa na baba, akisikia wenzake wanaita baba anapata uchungu na hata alipomuuliza mama yake hakumuelezea vizuri juu ya nani ni baba yake na wapi alipo.

Kauli ya Arima ikatufikisha kwa Afisa Malezi Ester Taji, hapa tulitaka kujua inakuwaje mpaka mzazi mmoja anamsemea mwenzie mabaya kwa mtoto?

Taji anajibu kuwa, “mara nyingi mafarakano ya wazazi huleta uhasama kwa Watoto kwasababu mzazi anayelea huwa anaongelea mambo hasi na hio husababishwa na kuona kumsema vibaya ni sehemu kutafuta Faraja na kusisitiza kuwa kusema madhaifu ya mwenza wako ni udhaifu mkubwa.”

Tafiti zinaonesha kuwa watoto wengi wa ‘single mama’ huzaliwa na kulelewa katika mazingira yasiyo rafiki na hivyo hupata malezi yenye upungufu.

Watoto hawa wengi wao huwa hawana nidhamu, hawafuatilii masomo, watoro shuleni na wengine huingia mtaani na kujihusisha na matumizi ya vilevi au uhalifu mwingine ambao huwapelekea kuingia matatani.

Kwa Wasichana wao huwa katika hatari ya kubeba mimba za utotoni na wengi wao kwa pamoja huishi kwa unyonge, upweke na wengine hupatwa na sonona.

Ijapokuwa mwanamke au mwanaume anaweza kulea mtoto peke yake, bado imeonekana Wanawake wengi ndio wanaolea watoto peke yao kwa asilimia kubwa, na hii hutokana na tafiti zinaonesha kwamba hadi kufikia 2050 nusu ya Wanawake wote Duniani watakuwa SINGLE MOTHERS, hivyo juhudi za kielimu, kidoni na gata binafsi zinahitajika ili kunusuru Taifa lenye ukosefu wa maadili hapo baadaye.

Muliro: Tunafuatilia, tunachunguza kupotea kwa Maclean Mwaijonga
Ruto ampa somo Kindiki, ataka ajiepushe na siasa za ukabila