Wanawake wametakiwa kusimamia kikamilifu jukumu la msingi la malezi ya watoto huku wakiendelea kujikita katika shughuli za kiuchumi, ili kudhibiti na kukomesha vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto katika jamii.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoani Geita Mrakibu Msaidizi wa Polisi Grace Kaijage wakati akitoa elimu ya ukatili katika jukwaa la Mwanamke Pambe, lililoandaliwa kujadili fursa za maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa wanawake.
Amesema, “dhamira ya vikundi hivi kwa akina mama inalenga kujikwamua kiuchumi, vikundi hivi vitumike kuondoa ukatili wa kijinsia katika jamii. Matukio mengi ya ukatili huanzia nyumbani na mara nyingi hutokea Mama hayupo. Usalama wa watoto ni malezi na siyo kuwajengea mageti.”
Naye Diwani wa Viti Maalum, Maimuna Mingisi amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuendelea kutoa elimu katika jamii huku akiwasisitiza Wanawake kusimamia malezi ya watoto, ili kudhibiti matukio ya ukatili na unyanyasaji.