Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Miguta Kibilu wa Kikosi cha usalama Barabarani Wilaya na Mkoa wa Singida amewataka Madereva kuzingatia sheria na kulipa madeni ya bila kushurutishwa baada ya kuandikiwa faini.
Kibilu ameyasema hayo wakati akiongoza operesheni ya kukamata magari mabovu na ukusanyaji wa madeni kwa madereva na wamiliki wa magari ambao wamekaidi kulipa madeni yao kwa hiari, na kuwataka kulipa madeni hayo kama taratibu zinavyowataka ili kuondoa usumbufu usio wa lazima.
Aidha, Miguta amekemea tabia ya baadhi ya Madereva ya kuchanganya abiria na mizigo jambo ambalo linahatarisha usalama wa abiria wawapo safarini kwani mizigo mikubwa inaweza kupelekea gari kukosa uwiano mzuri na kusababisha ajali.
Katika operation hiyo, jumla ya magari 24 yaliyokaguliwa yalibainika kuwa na makosa mbalimbali ambapo yaliadhibiwa kwa kuandikiwa faini, ili waende kuyafanyia marekebisho tayari kwa kuendelea kutoa huduma yakiwa katika hali nzuri.