Dimba la Tanzanite Babati linakwenda kuwaka moto jioni ya leo kwa mchezo unaowakutanisha Fountain Gates dhidi ya Pamba jiji. Huu ni mchezo wa 11 kwa timu hizo na kila moja ina mtazamo wake. Fountain Gates inashika nafasi ya 5 kwenye msimamo wa ligi na kama itashinda mchezo huo itafikisha alama 20 na kuendelea kusalia katika nafasi hiyo.
Klabu hiyo imekuwa na mwenendo mzuri tangu mwanzo wa ligi. Uwepo wa Salum Mwalimu unawapa ujasiri wa ushindi katika mchezo huo muhimu. Kwa upande wa Pamba Jiji wao wamekalia kuti kavu mpaka sasa wakiwa na alama 5 pekee katika michezo 10 waliyocheza wakishika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi.
Ujio wa Kocha Fredrick Minziro aliyechukua nafasi ya Goran Kopunovic haujazaa matunda chanya mpaka sasa baada ya kuiongoza Pamba Jiji katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar na kutoka sare ya bao 1-1 na kisha kupoteza michezo miwili kwa bao 1-0 dhidi ya Tabora United na Namungo.
Kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Azam FC kiliendelea kumpa wakati mgumu kocha Minziro na kumwekea rekodi mbaya ya kucheza michezo minne akifungwa michezo mitatu na sare 1 huku akiruhusu mabao 5 na yeye kufunga bao 1 pekee. Swali ni je Minziro atakuja na mbinu gani katika mchezo huo muhimu na kipi afanye kurudisha imani na ari ya ushindani klabu hapo.
Kama Pamba jiji wataibuka na ushindi katika mchezo huo watafikisha alama 8 sawa na kagera sugar walio nafasi ya 14. Uongozi wa Pamba una jukumu kubwa sana kumsaidia mwalimu minziro kurejesha matumaini ya wanamwanza.