Afisa elimu Taaluma Mkoa wa Arusha, Mwalimu Shirley Swai amewataka vijana kuendelea kushirikiana na kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Jeshi la Polisi katika kuzuia matukio ya uhalifu katika maeneo yao.
Mwalimu Swai alitoa wito huo wakati akimwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Arusha kwenye Fainali za Mashindano ya Arusha Polisi Jamii Cup 2024 yaliyofanyika katika viwanja vya Don Bosco vilivyopo katika chuo cha KIITEC Jijini Arusha.
Mbali na kulipongeza Jeshi la Polisi kwa namna ambavyo wamekuwa wakijitahidi kutumia njia mbalimbali kuzuia uhalifu, alisema endapo vijana watatoa ushirikiano kwa Polisi basi changamoto ya uhalifu itapungua kama sio kuisha kabisa.
Kwa upande wake Afisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi Debora Lukololo ambaye alimwakilisha Kamanda wa Polisi aliwasihi vijana kutumia michezo kuhimizana kujiepusha na vitendo vya mmomonyoko wa maadili ikiwa ni pamoja na matumizi ya dawa za kulevya, mapenzi ya Jinsia moja sambamba na kujiepusha na makundi mabaya.
Aidha aliwakumbusha vijana hao kushiriki uchaguzi ambao utafanyika Novemba 27 mwaka huu kwa ajili ya kuchagua viongozi ngazi za mitaa, ambapo aliwataka kujiepusha na vitendo vya uhalifu katika mchakato mzima wa uchaguzi kuanzia wakati wa kampeni.
Naye Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi, Peter Lusesa alisema lengo la mashindano hayo pamoja na mambo mengine ni kuimarisha ushirikiano mzuri baina ya Jeshi la Polisi na wananchi ili kubaini changamoto mbalimbali za kihalifu katika Jamii na kuzitafutia majawabu.
Aidha, alitoa wito kwa vijana hao kutumia muda wao vizuri kushiriki katika masuala mbalimbali ya kijamii ikiwemo kufanya kazi kwa ajili ya kujipatia kipato halali, kufanya mazoezi, kutoa taarifa za uhalifu, kushiriki katika vikundi vya ulinzi shirikishi kwaajili ya kuimarisha ulinzi na Usalama katika maeneo yao.

Waziri Kombo asisitiza utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi
Equatorial Guinea: Waliofanya mapenzi ofisi za Umma kutimuliwa