Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo ametembelea Ofisi za Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Cuba na kuzungumza na watumishi wa ubalozi huo jijini Havana.
Akizungumza na watumishi hao Balozi Kombo amewataka wafanye kazi kwa bidii, waledi na ubunifu ili waweze kutekeleza kikamilifu malengo waliyopewa kuyakamilisha katika kituo hicho kwa niaba ya Serikali hususan utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kwa kuzinadi fursa mbalimbali zinazopatikana nchini kama vile biashara, uwekezaji na utalii.
Pamoja na masuala mengine Balozi Kombo amewapongeza watumishi hao kwa mapokezi ya ujumbe wa Tanzania unaoendelea kuwasili jijini Havana pamoja na maandalizi ya maeneo mengine yatakayohusika na Ziara ya Kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwemo maandalizi ya ukumbi wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili linalotarajiwa kuwa na washiriki wapatao 400 litakalofanyika jijini Havana tarehe 8 Novemba 2024.
Aidha, Waziri Kombo alitumia wasaa huo pia kutembelea eneo la Ubalozi sambamba na kujadili changamoto mbalimbali zilizopo katika kituo hicho na kuahidi kuzitafutia ufumbuzi mapema ili kuuwezesha ubalozi huo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Waziri Kombo yupo nchini Cuba kukamilisha maandalizi ya Ziara ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini humo ambapo ameeleza moja ya mafanikio ambayo ubalozi huo unatakiwa kuona fahari ni jitihada ilizozitumia kufanikisha Kongamano la Kimataifa la Kiswahili kufanyika nchini humo kwakuwa, litawezesha kufikia lengo la Seriakali la kuzitaka Balozi kukibidhaisha Kiswahili kikanda na kimataifa.