Na Faudhia Simba, Dar24 Media – Dar es Salaam.

Anaitwa Sushant Singh Rajput, alikuwa ni mwigizaji wa Kihindi anayejulikana kwa kazi yake ya kucheza Sinema ya Kihindi akiigiza katika filamu kadhaa za Kihindi zilizofanikiwa kibiashara kama vile M.S. Dhoni, Kedarnath, The Untold Story, Kai Po Che, Chhichhore nk, kiasi ilimpelekea kupata Tuzo kadhaa na hata kuteuliwa kuwania Tuzo za Filamu mara tatu.

Alizaliwa January 21, 1986 huko Mumbai nchini India na kusoma Shule ya Kalanchi Hansraj kisha kuja kumaliza chuo Cha Delhi technology kilichopo  New Delhi lakini wakati wote huo alikuwa na ndoto yake moja tu iliyo kubwa nayo si nyingine ila ni uigizaji.

Uigizaji.

Inaarifiwa kuwa sio rahisi kwa nchi ya India mtu ambaye hajatoka kwenye familia ya waigizaji akapata nguvu, ujasiri Hadi kuonekana na Kila mtu kupenda kazi yake kwani usipotoka kwenye familia ya uigizaji ni ngumu kuja kukubalika lakini shushant Singh Rajput alipambana.

Sushant akawa ni mmoja wa waigizaji waliofuatiliwa sana, waliopendwa, akisifiwa kwa unyenyekevu, na wenye vipaji ndani ya Bollywood, ambapo haikuwa na ubishi kwamba alitarajiwa kuwa nyota mkubwa wa Bollywood anayefuata kutokana na sifa zake hizo mujarab.

Changamoto.

Kama ilivyo katika kila kazi hakukosi changamoto, basi naye alikumbana  na hili jambo kwani kazi zake nyingi zilikuwa zikifungiwa bila sababu za msingi na nyingine zilikuwa hazitoki ila ilihisiwa kuwa ni sababu ya ubaguzi kwani vikwazo vilikuwa ni vingi lakini bado alitumia muda wake kufanya anachokipenda.

Hata hivyo, kuna kipindi mashabiki wake walikuwa hawamuelewi na kumjia juu kwa hasira kutokana na movie zake ambazo anaigiza asilimia kubwa mwisho wa stori lazima afe, na kuna siku sijui moja shabiki wake alitoa lake la moyoni kuhusu hilo kwa kumuandikia ujumbe kwenye mitandao yake ya kijamii.

“Sitazami Tena filamu zako sababh Kila movie unakufa naamini kwenye filamu mpya ambayo umeigiza pia unakufa,” aliandika shabiki huyo kwa hasira, lakini Shushant alimjibu kwa hekima kuwa, “tafadhari naomba usiache kutazama filamu zangu, stori ndio zinataka hivyo.”

Kifo chake.

Kwa bahati mbaya, malengo yake yote ya maisha na ndoto zake zilifikia kikomo alipopatikana amekufa katika nyumba yake ya Bandra Juni 14, 2020, akiwa na umri wa miaka 34 na hata baada ya miaka minne tangu kifo chake, watu bado walikuwa hawataki kuukubali ukweli kutokana na tabia zake za kuigiza kufa.

Ilikuwa ni wakati wa kuvunja moyo kwa sehemu kubwa ya jamii, kwani watu walikasirika sana, na kuzaliwa kwa harakati kubwa ya “Boycott Bollywood” kwani kifo chake kiliibua mijadala ya kwamba kulikuwa na upendeleo ndani ya Bollywood kwa kuwajali Watu wa nje dhidi ya watu wa ndani.

Mambo mengi yalitokea, lakini yote hayo sasa ni historia, isipokuwa familia ya Sushant na mashabiki wake wakubwa bado wanapigania haki, ikionekana kuwa moja ya sababu kubwa ni mtu kumpenda Sushant Singh Rajput ni tabia yake ya kujali na kutomdharau mtu yeyote katika maisha yake ya kazi ya uigizaji.

Alijulikana kwa kuwaheshimu wakubwa wake na kuwaongoza wadogo kwake, ingawa inasemwa kwamba sababu ya kifo chake ni msongo wa mawazo lakini pia inahisiwa alitumia dawa za kulevya na hata kabla ya kifo shushant Singh anadaiwa kuwa alipiga simu kwa watu wake wa karibu lakini hakuna ambaye alipokea.

Hisia mseto.

Inadaiwa hata mpenzi wake, Ankita Lokhande naye hakupokea simu yake, hivyo ikasemwa kwamba huwenda kuna jambo alitamani kuwashirikisha kabla ya kufanya maamuzi hayo, kwani ni mtu ambaye alikuwa na msongo wa mawazo kwa muda mrefu na hakupata tiba.

 

Tukio jingine ambalo bado limeacha maswali ni kuwa, kabla ya kifo cha Shushant siku kadhaa nyuma Meneja wake pia alifariki kwa kujiua bila watu kujua nini chanzo, lakini kwa Shushant familia iliingilia kati na kufungua kesi juu ya suala hili, ikisema vipimo havikuonesha kuwa alitumia dawa zozote ikiwemo za kulevya.

Hata hivyo, kesi hii ilitupiliwa mbali baada ya familia ya Shushant Singh kuwashinikiza Madaktari kuhusu majibu ya ndugu yao, licha ya ripoti ya kusema mbali na kujinyonga pia inaonekana Star huyo wa Filamu alitumia dawa, lakini wao walikuiwa wakishuku kuwa ameuliwa.

Mashabiki waingilia kati.

Hili hiyo halikuishia hapo, kwani mashabiki nao hawakutaka kuelewa moja kwa moja walimnyooshea kidole Salman Khan wakidai ndiye alihusika na kifo cha msanii huyo, hii ni baada ya Shushant Singh kumzungumzia Soraj panchol mtoto wa Aditya Panchol ambaye ni rafiki mkubwa wa Salman Khan.

Shushant Singh Rajput alisema, “kuwa kijana ni maarufu sababu ya jina la baba yake, hivyo ndivyo ilivyo kwa waigizaji wengi wa India.” Kauli hii ilimchukiza Salman Khan na alipompigia simu Shushant akifoka kwa hasira, jazba na maneno makali ambayo yalipelekea mashabiki wa Shushant kudai Salman ndiye muhusika wa mauaji kwani alimtishia maisha.

Hata hivyo, Salman Khan aliwataka mashabiki wake wasiingie kwenye mtego wa kugombana na mashabiki wa Shushant kwani anaelewa hali ambayo wanapitia kwa wakati huo, kauli ambayo ilionesha wazi kuwa Shushant Singh alikuwa na tatizo na Salman Khan lakini huenda walimaliza tofauti zao.

Hili lilikuja kuthibitishwa mwaka 2017, kupitia ripoti ya Filmfare iliyoibua tafrani katika tasnia ya filamu, baada ya kudai kwamba Salman Khan alimkaripia Sushant Singh Rajput kwenye simu na mara tu ripoti hiyo ilipouafikia Umma, watu walianza kuwa na wasiwasi kuhusu maisha ya uigizaji ya Sushant ndani ya Bollywood, kwani kila mtu alikumbuka kisa cha Vivek Oberoi.



Sababu za Salman kumkaripia Sushant.

Kwa mujibu wa ripoti ya Filmfare, inadai kuwa Sushant Singh Rajput na Sooraj Pancholi, walikutana Desemba 2017 kwenye sherehe na wakati wakizungumza, Sushant alidaiwa kumkosea heshima kijana Sooraj bila sababu yoyote.

Ripoti hiyo, iliongeza kuwa hata Sooraj Pancholi mwenyewe alishangazwa na tabia mbaya ya Sushant kwani hakuwa amefanya chochote kumchokoza na mara baada ya suala hilo kumfikia baba wa kijana huyo (Salman Khan), naye alichukua hatua bila kufikiri kitakachotokea mbele na hali hiyo iliongeza zaidi utata.

Sushant aomba samahani.

Kwa mujibu wa ripoti ya Filmfare, inaeleza kuwa Salman Khan alimpigia simu Sushant Singh Rajput na kumuonya akae mbali na kijana wake, Sooraj Pancholi lakini inasemekana kwamba Sushant alijishuka na kukubali makosa yake kisha kumuomba msamaha Salman kwa alichomfanyia Sooraj.



Ndipo hali ilitulia na baadaye walionekana wakiwa pamoja Sushant Singh Rajput na Salman Khan kwenye kipindi cha Bigg Boss cha matukio ya filamu na sherehe kwenye luninga moja Nchini India ingawa baadhi ya watu walibeza kuwa hiyo ilikuwa ni geresha tu ila ukweli ni kuwa kuna tatizo kati yao.

Uthibitisho wa Kifo.

Baada ya ripoti za kifo chake, Polisi wa Mumbai walithibitisha kuwa mwili wake ulipatikana nyumbani kwake Bandra, hapo akatafutwa msemaji wa familia ya Sushant ambaye alinukuliwa akisesema, “inatuuma kusema kwamba Sushant Singh Rajput hayupo nasi tena.”

“Tunawaomba mashabiki wake wamuweke katika mawazo yao na washerehekee maisha yake, na kazi yake kama walivyofanya hadi sasa. Tunaomba vyombo vya habari vitusaidie kudumisha faragha wakati huu wa huzuni,” alisema Nitesh Tiwari.

Upelelezi wa Kifo.

Miezi miwili baada ya kufariki kwa Sushant Singh Rajput, Mahakama Kuu Nchini India iliiteua Ofisi Kuu ya Upelelezi (CBI) kuchunguza kesi hiyo na baada ya siku kadhaa za uchunguzi wa kesi hiyo maafisa hao walisema hawajapata ushahidi wowote wa kuuawa kwa Rajput.
Ofisi nyingine ya IWC ikaamua kuichukua kesi hiyo kutoka kwa Polisi wa Mumbai, yenyewe ikaja na jibu kuwa imepatiwa ushahidi wote uliokusanywa na hata kujenga upya eneo la kifo chake, ambapo wakawahoji watuhumiwa muhimu akiwemo Muigizaji Rhea Chakraborty aliyehojiwa kwa jumla ya masaa 35.

Utata wa Taarifa.

Bado mpaka sasa kifo cha Sushant Singh Rajput kimewagawa watu, wapo wanaoamini kuwa alijiuwa na wapo wanaendelea kuamini kuwa aliuliwa, lakini katika upelelezi ilionekana kuwa taarifa za kibenki za Sushant Singh Rajput zilionesha kuwa gharama kubwa zilitumiwa na aliyekuwa mpezi wake Rhea Chakraborthy.

Sushant Singh Rajput alikuwa na zaidi ya Rupia 46 mwezi wa Novemba 2019 na zilipungua hadi zaidi ya cr 4 katika mwaka 2020 na ikionesha kwamba kuna matumizi ya tiketi za Ndege za Rupia 81K ya Showik Chakraborty huku gharama kubwa zikiwa ni za kibinafsi za Rhea Chakraborty.

Samee Ahmed aliyekuwa mkufunzi wa mazoezi wa Sushant sighn Rajput alizungumza na chombo kimoja cha Habari na kudai kuwa, “Sushant aliniambia kwamba alikuwa anachukua dawa ya Dengue. Hakuweza kujikita zaidi kwenye Workout kutokana na dawa hizo.”

Samee Ahmed Aliendelea kwa kusema kwamba “Sushant alikuwa mtu aliyebadilika baada tu ya kuwa na Rhea Chakraborty kwani alianza kuchukua dawa za kushangaza tangu Desemba 2019. Vidonge vilikuwa na athari hasi na Miguu yake ilianza kutetemeka na Sushant hakuwahi kunywa vidonge kabla ya kukutana na Rhea.”

Hitimisho.

Ni wazi kuwa kila mtu ana ndoto na kutamani afike mbali au anatamani kuyafikia malengo yake maishani, lakini wote huwa na njia tofauti wengine wakiamini katika Magari, wengine Nyumba, wengine Mpira, wengine Kilimo, wengine Urembo nk ambapo bidii zao huwapa mafanikio ingawa ukweli ni kuwa hakuna aliyewahi kuridhika nayo.

Lakini kwa Sushant yeye aliamua kuwekeza kwenye kipaji chake cha kuigiza, siwezi kusema kwamba aliyafikia mafanikio yake ama la, lakini kwa sehemu alifanikisha na hata sasa jina lake halitasahaulika katika ulimwengu wa Filamu kwa ukubwa Nchini kwake India.

Hivyo tuna sababu kubwa ya kuhakikisha kwamba tunakiamini kile tunachopambania kama somo kutoka kwa muigizaji huyu nguli, ambaye kesi yake bado ina utata na haina hitimisho sahili kuweza kueleza ni ama aliuliwa, ama alijiuwa hili linabaki fumbo na ukweli anaweza kuuthibitisha yeye mwenyewe, lakini sasa hayupo tena Duniani na huenda wale waliopigiwa simu labda wangeambiwa kinachomsibu hivyo tubaki tu kusema kifo ni fumbo.

Elimu: Waonywa kutojihusisha na mapenzi Shuleni
Cuba: Waziri Kombo atembelea makumbusho ya Fidel Castrol