Uzinduzi wa Tuzo ya uwiano wa kijinsia kwa Vyombo vya Habari “Media for Gender Equity Awards” yenye ujumbe unaosema “Kalamu Yangu, Mchango Wangu kwa Wanawake” umetangazwa rasmi na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar – TAMWA ZNZ.
Kupitia taarifa yake iliyotolewa hii leo Novemba 7, 2024 kwa Vyombo vya Habari, imeeleza kuwa Tuzo hiyo itatambua vyombo na Waandishi wa Habari Zanzibar wanavyoandika habari za kina kuhusu mafanikio, changamoto, michango ya wanawake katika uongozi, na vinavyoshiriki kikamilifu katika kukuza usawa wa kijinsia kupitia kazi zao.
TAMWA ZNZ ambayo imeshirikiana na Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na Jumuiya ya mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO), imesema kupitia tuzo hiyo, wanalenga kuhamasisha Vyombo vya Habari na Waandishi kuunga mkono sauti za wanawake.
Malengo mengine ni kukuza uandishi wa habari wenye kuzingatia usawa wa kijinsia ili kuchangia mabadiliko ya kijamii kwa kuonesha nafasi za wanawake na uwezo wao katika uongozi ili kuleta maendeleo, wakilenga pia kutambua vyombo vya habari vyenye mtiririko mzuri wa kusaidia kuongeza wanawake katika nafasi za uongozi.
“Hivyo vigezo vitakavyotumika ni kuwa na sera ya kijinsia, dawati la kijinsia, zana za tathmini na ufuatiliaji wa masuala ya usawa wa kijinsia, idadi ya habari zilizoandikwa kuhusu wanawake na uongozi na nafasi ya wanawake waandishi wa habari katika chombo cha habari,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, imefafanuliwa kuwa, “Mradi wa SWIL uliwahi kuwapa mafunzo na kusaidia vyombo vya habari 11 kutoka Unguja na Pemba kuandika na kuweka kumbukumbu na kufanya ufuatiliaji na tathmini katika kipindi cha mwaka 2022 hadi 2023. Hivyo tunaamini kuna vyombo vimeweza kuleta mabadiliko makubwa na vinahitaji kutambuliwa na kuthaminiwa.”
“Tuzo hii, itahusisha kazi zilizotolewa na Waaandishi wa Habari katika Vyombo vya Habari vya aina nne kama ifuatavyo:
Uandishi wa habari za Makala katika magazeti (feature articles). Uandishi wa habari wa vipindi katika redio (radio program). Uandishi wa habari katika Televisheni (TV program). Uandishi wa habari wa makala katika mitandao ya kijamii (feature articles in social media story),” ilifafanua taarifa hiyo.
Aidha, imetaja vigezo muhimu vya kuzingatia kuwa ni ubora wa kazi iliyowasilishwa, upekee wa mada, umuhimu wa kuzingatia uwiano sawa wa jinsia, vyanzo vingi vya habari vilivyojitawanya, ubunifu wa mada husika, ufasaha na mtiririko wa lugha, matokeo baada ya kutoka habari au kipindi hicho (impact), uwasilishaji wa mada husika, mpangilio wa mada, kuzingatia maadili ya uandishi wa habari na weledi na matumizi ya TAKWIMU.
Taarifa ya TAMWA ZNZ imezidi kufafanua kuwa, kipindi cha Redio na Television kisizidi dakika 30 na pia sauti na picha ziwe katika ubora unaostahiki na kipindi au makala iliyochapishwa au kurushwa katika vyombo mbalimbali vya habari vikiwemo magazeti, runinga, redio na mitandao ya kijamii katika kipindi cha kuanzia Januari 1 hadi Disemba 31, 2024.
Kama ilivyokuwa kwenye vyombo vya habari SWIL, imeeleza kwamba ilikaa na waaandishi wa habari 170 kwa mafunzo na majadiliano kuhusu kuandika habari nzuri za wanawake na uongozi. Kiasi cha waandishi wa habari 45 wametambuliwa kwa kuandika habari za kuongeza ushiriki wa wanawake kuanzia 2021 hadi 2023.
Mchakato wa Uwasilishaji na Vigezo vya Tathmini Dirisha la kupokea kazi liko wazi kuanzia kwa waandishi wa habari kutoka vyombo vya habari mbalimbali Zanzibar, ikiwemo magazeti, televisheni, redio, na mitandao ya kijamii huku jopo la majaji, likiwa na wataalamu wa uandishi wa habari na utetezi wa kijinsia, litapitia kazi za vyombo vya habari na za waandishi wa habari mapema Januari baada ya kukamilika kwa zoezi la ukusanyaji kazi.
Imesema, maombi yamefunguliwa rasmi hii leo na kazi zitaendelea kupokelewa hadi Januari 5, 2025 na kwamba Waandishi wa habari wanaweza kuwasilisha kazi zao ambazo zimezalishwa kuanzia Januari hadi Disemba, 2024 moja kwa moja Ofisi za TAMWA ZNZ zilizopo Tunguu na Mkanjuni Chakechake Pemba, au kupitia barua pepe ya
info@tamwaznz.or.tz na kiungo/link itakayotumwa kwenye mitandao ya kijamii.