Afarah Suleiman, Babati – Manyara.
Kamati ya Utalii, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imeitaka Wizara ya Kilimo, Mifugo, Umwagiliaji, Mali Asili na Mifugo Zanzibar kuharakisha mchakato wa kuingia makubaliano na kampuni ya Mbolea Minjingu inayozalisha Mbolea asilia, ili kuachana na uagizaji wa Mbolea za Kemikali kutoka nje ya nchi inayohatarisha afya ya udongo.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mtumwa Pea Yusufu katika Kiwanda cha Mbolea cha Minjingu cha Mkoani Manyara baada ya Kamati hiyo kutembelea Kiwanda hicho kwa lengo la kujifunza ubora wa mbolea hiyo rafiki kwa Mazingira.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo, Umwagiliaji, Mali Asili na Mifugo Zanzibar, Ali khamis Juma ambaye aliambatana na Kamati hiyo amesema tayari Wizara yake imetoa bure maghala manne kwa Kampuni ya Minjingu kuhifadhi mbolea Zanzibar, ili kurahisisha usambazaji wa mbolea hiyo asilia kabla ya Januari 2025.
Lengo la Wizara ya Kilimo, Mifugo, Umwagiliaji, Mali Asili na Mifugo Zanzibar ni kupunguza uagizaji wa mbolea za kemikali viwandani kwa zaidi ya asilia 50 kuanzia Januari 2025.