Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi – CCM, (NEC), Itikadi Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, amewaomba wanachama katika maeneo ambayo wagombea wa CCM wamewekewa mapingamizi, kuwa watulivu kwani Chama kinaamini haki itatendeka kwa vyama vyote.
 
Makalla aliyasema hayo leo wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, ambapo amesisitiza CCM kitaibuka na ushindi wa haki katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.

 

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla. 

“Niwaombe wanaCCM, tupo katika hatua za mapingamizi. Sasa hivi kinachoendelea mitandaoni ni malalamiko ya vyama vya upinzani kuonyesha kama vile pekee ndiyo waliowekewa mapingamizi.
 
“Wanafanya hadaa, upotoshaji wa takwimu feki na kujisahaulisha kwamba hata wagombea wa CCM wamewekewa mapingamizi. Juzi nilisema tunaamini TAMISEMI itatenda haki kwa vyama vyote kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki na atakayeshinda atangazwe kwa haki,” alisema Makalla.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla akizungumza na Wanachama pamoja na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Mkuranga katika Uwanja wa CCM Wilaya ya Mkuranga.

“Kwa hesabu zetu na wagombea tuliowaweka, tunaamini CCM tutashinda kwa haki. Kwa hiyo rufaa zinaendelea, baada ya uteuzi wa wagombea CCM kitatoa taarifa baadaye.”
 
Makalla alikemea tabia hiyo ya baadhi ya vyama vya upinzani kupotosha umma kwamba wagombea wa vyama hivyo pekee, ndiyo wamewekewa mapingamizi, wakati si kweli. 

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla , akikabidhiwa baiskeli na Mbunge wa Jimbo la Mkuranga na Waziri wa Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ili kuwagawia Viongozi wa Malawi ya CCM 250 katika jimbo hilo.

Alisema kuwa vyama vyote, kikiwemo CCM, ambavyo wagombea wake wamewekewa mapingamizi ya kuteuliwa, vinaendelea kukata rufaa, kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa. 
 
“Niwaombe wanaCCM katika maeneo ambayo tumewekewa mapingamizi, tuwe watulivu tukiamini haki itatendeka kwa vyama vyote,” alisisitiza CPA Makalla.

Yanga wakalia kuti kavu mambo yamezidi kuwa magumu kila kona
Afya ya Msingi: Tathmini ya usimamizi kila baada ya wiki mbili