Wizara ya Afya Nchini Lebanon, imesema takribani watu 23 wengi wao wakiwa ni Wanawake na Watoto, wameuawa kufuatia mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Israel eneo la Joun na Baalchmay lililopo Mlima Lebanon katikati mwa Taifa hilo, ambako kundi lenye silaha la Hezbollah huweka makazi yake hapo.
Kufuatia shambulizi hilo, Jeshi la Israel limesema lilikuwa likichunguza taarifa hizo huku taarifa nyingine ikidai kuwa pia watu wawili waliuawa kutokana na kurushwa kwa roketi ya Hezbollah katika mji wa Nahariya kaskazini mwa Israel.
Tukio hili linakuja ikiwa ni siku moja baada ya Waziri wa Ulinzi wa Israel kukataa kusitisha mapigano na Hezbollah, likisema linataka kuhakikisha linarejesha usalama wa eneo la mpaka wa kaskazini mwa Israel.
Zaidi ya watu 3,200 wameuawa nchini Lebanon tangu kuanza kwa mashambulizi, ikiwa ni pamoja na wale 2,600 katika wiki saba tangu Israel ianzishe kampeni ya anga ambapo Watu milioni 1.2 tayari wameyahama makazi yao.