Jeshi Ia Polisi Mkoa wa Iringa linachunguza tukio la mauaji ya Katibu wa Chama Cha Mapinduzi – CCM, Wilaya ya Kilolo, Christina Nimrod Nindi (56) ambaye alifariki baada ya kushambuliwa kwa kupigwa risasi kifuani pamoja na kupigwa na kitu kizito kichwani na watu wasiofahamika.

Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi ambayo imetolewa hii leo Novemba 13, 2024 kwa vyombo vya Habari imeeleza kuwa Christina ambaye alikuwa ni mkazi wa Kitongoji cha Banawanu, Kijiji cha Ugwachanya, Kata ya Mseke Tarafa ya MIoIo alifariki Novemba 12, 2024 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Tosamaganga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi.

“Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa marehemu alivamiwa na vijana watatu wasiofahamika katika nyumba anayoishi na binti zake wawili. Pia watu hao walimshambulia binti mmoja wa marehemu na kumuumiza usoni pamoja na jirani yake ambaye naye ameumizwa eneo la ubavu wa kushoto kwa kupigwa na kitu butu alipokwenda kutoa msaada baada ya kusikia kelele kutoka kwa binti wa marehemu,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kamanda Bukumbi amesema, baada ya kufanya shambulio hilo, watu hao walitoroka na hawakuchukua chochote na kwamba Polisi inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kuhakikisha watuhumiwa wanapatikana na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Bukoba: Uchafuzi wa Mazingira wamkera Diwani, Meya atoa kauli
Daraja la Muhoro litawainua Watanzania kiuchumi - Runji